Na Clara Matimo, Mtanzania Digital
Wanawake wanaoishi maeneo ya vijijini katika Mkoa wa Mwanza, Manyara na Arusha wamehamasishwa kumiliki ardhi kisheria ili wawe na nguvu ya kiuchumi itakayowawezesha kuepuka vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Wito huo umetolewa na wadau wa masuala ya wanawake katika muendelezo kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini yaliyofanyika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza Kijiji cha Mhungwe, Babati Mkoa wa Manyara Kijijini Magugu na Arusha Wilaya ya Arumeru Kijiji cha Kikatiti yakilenga kutoa semina kuhusu kuielimisha jamii haki ya mwanamke kutumia na kumiliki ardhi, kuzuia ukatili wa kijinsia, uchumi na kujikinga na ugonjwa wa Uviko 19.
Wadau hao ni Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa kushirikiana na mashirika mbali mbali yasiyo ya Serikali likiwemo Shirika la Tahea linalojishughulisha na masuala ya elimu, afya, kilimo na uchumi wa nyumbani, Mwanza Rural Housing Propgamme (MRHP) na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) ambao walianza msafara wa kijinsia Oktoba 12 kutoka jijini Mwanza wakielekea Mkoani kilimanjaro kuhudhuria kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika kitaifa Oktoba 15 kwa ufadhili wa Shirika la We Effect linalojishughulisha kuboresha makazi ya watu wanaoishi katika makazi duni lenye makao yake jijini Nairobi nchini Kenya.
Msafara huo wa kijinsia kuelekea siku ya mwanamke anayeishi kijijini wenye kauli mbiu ’Ardhi ni nyenzo ya maendeleo kwa mwanamke wa kijijini’ unapita katika vijiji mbalimbali ukiwapa pia wanawake mbinu za kujikimu kimaisha, ujasiliamali na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye maadhimisho hayo, katika vijiji mbalimbali, Mratibu wa TAWLA), Mkoa wa Mwanza, Wakili Fatuma Kiwanga, alisema mwanamke akimiliki ardhi itamsaidia kujikwamua kiuchumi maana anaweza akaitumia kupata mkopo katika taasisi mbalimbali za fedha ambazo zitamsaidia kufanya biashara hivyo kuweza kumudu mahitaji yake na familia jambo ambalo litapunguza kunyanyaswa.
“Niwasishi sana wanawake wenzangu, kila mwenye nafasi ya kiuchumi amiliki ardhi kisheria ili imsaidie, nafasi hiyo tunayo wanawake wote tuondokane na mitazamo hasi ya zamani kwamba mwanamke hawezi kumiliki ardhi kila mtanzania anahaki kikatiba ya kumiliki arhi kwa kufuata taratibu zilizowekwa sheria ya ardhi namba nne na tano ya mwaka 1999 zinaelezea usawa wa kijinsia katika kumiliki ardhi tusibaki nyuma wanawake maana wanawake ndiyo nyenzo muhimu katika uzalishaji mali,”alisema.
Kiongozi wa msafara huo wa kijinsia, Janeth Shishila, ambaye ni Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Mwanza, amesema serikali kupitia idara ya maendeleo ya jamii inatambua umuhimu na thamani ya mwanamke anayeishi kijijini hivyo imeona ipo haja kuungana na wadau hao wa masuala ya wanawake kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini kutoa elimu itakayomuwezesha kumiliki ardhi kisheria, kujikinga na janga la Uviko 19, kukumbushana umuhimu wa usawa wa kijinsia katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo jumuishi kama ambavyo imesisitizwa katika dira ya maendeleo ya mwaka 2025.
“Kauli mbiu ya msafara huu inayosema ‘Ardhi ni Nyenzo ya Maendeleo kwa Mwanamke wa Kijijini’ inalenga kuhamasisha uwajibikaji kwa wadau wote wa maendeleo kuanzia ngazi ya taifa hadi mtaa kwa sababu inamgusa kila mwanamke anayeishi kijijini maana shughuli kuu ya kiuchumi ni kilimo na wanawake ndiyo hushiriki shughuli hiyo kwa asilimia kubwa ndiyo maana tunapita maeneo mbalimbali kutoa elimu tunabaini changamoto walizonazo wanawake ili baadaye serikali izifanyie kazi,”alisema Shishila.
Naye Meneja Mradi wa Uboreshaji nyumba na makazi kutoka Tahea, Musa Masongo, alizitaja changamoto mbalimbali zinazomkabili mwanamke anayeishi kijijini kuwa ni kubeba majukumu makubwa ya kufanya kazi za nyumbani, mitaji midogo ya biashara isiyojitosheleza, ushiriki mdogo katika matumizi na usimamizi wa ardhi kutokana na mila na desturi zilizopo katika jaamii kuanzia ngazi ya familia na ukatili wa kijinsia ambapo wanawake wamekuwa wakipata vipigo, kubakwa na unyanyasaji mwingine.
“Naiomba serikali imuangalia mwanamke anayeishi kijijini kama nyenzo ya kiuchumi pia itoe elimu mara kwa mara kutumia njia tofauti tofauti ili kufikisha ujumbe kwa jamii na kuwajengea uwezo wanawake wanaoishi vijijini,”alisema Masongo.
Kwa upande wake Mhamasishaji Jamii Kutoka Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Mkoa wa Arusha(Mviwaarusha), Thomas Laiser, alisema kwa kujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO) wanawake wanaoishi vijijini wanachangia zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi mashambani katika mataifa yanayoendelea ikiwa ni sehemu ya kuchukua ajira kubwa zisizo na malipo kama kutoa huduma na kazi za nyumbani katika familia.
“Utafiti huo wa Fao wa mwaka 2017 ulibainisha kuwa ni wanawake vijijini wanaozalisha kati ya asilimia 60 hadi 80 ya chakula chote kinachozalishwa katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara Tanzania ikiwemo hivyo kutokana na mchango mkubwa wa kundi hili naiomba serikali kuhakikisha rasilimali zozote zinazopatikana kwa ajili ya kukabiliana na janga la Uviko 19 kuelekezwa vijijini kwa kufanya hivyo itakuwa ni njia sahihi ya moja kwa moja kulikinga kundi hilo la wazalishaji wakuu wa taifa na ugonjwa huo,”alisema Laiser.
Kauli ya serikali
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, Veronica Kessy, aliyewakilishwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Petro Musiba, Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, Karolina Mthapula na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dk. Athuman Kihamia, waliokuwa wageni rasmi katika maadhimisho hayo walisema serikali itaendelea kusimamia sera, sheria, mipango na mikakati mbalimbali ili kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kiuchumi, kijamii na kisiasa lengo likiwa ni kufikia usawa wa kijinsia.
Mthapula aliwataka wakazi wa Mkoa huo kutumia elimu waliyoipata kupitia msafara huo wa kijinsia kubadilika na kumthamini mwanamke kwa kuhakikisha anapata haki zake za kimsingi, kiuchumi na kijamii kwani Manyara ni mkoa wa pili kwa matukio ya ukatili wa kijinsia nchini.
Tanzania ilianza kuadhimisha siku ya mwanamke anayeishi kijijini mwaka 2008 ambapo huungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa Duniani lengo likiwa ni kujenga hamasa, mshikamano na uwezo wa wanawake waishio vijijini katika kushiriki na kunufaika na maendeleo ya kitaifa na kimataifa ambayo taifa limejiwekea katika kukuza uchumi na kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini mwaka huu inasema ‘Tujenge ustahimilivu kwa mwanamke anayeishi Kijijini katika kukabiliana na Uviko 19’.