27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wanawake wafuata nyayo za Malkia Sheba

Na Mwandishi Wetu, Mitandaoni

TAIFA la Ethiopia limerudi tena kwenye anga za kisiasa barani Afrika na duniani. Safari hii taifa hilo likichomoza na jina jingine la kiongozi mzito katika muundo wa utawala wake.

Kwa mara nyingine nafasi ya mwanamke katika utawala wa Ethiopia imepanda juu zaidi baada ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abiy Ahmed kumteua Birtukan Mideksa kuiongoza tume ya uchaguzi nchini humo.

Mwanamama huyo anaingia kwenye orodha ya wanawake wanaoshikilia madaraka ya juu zaidi nchini Ethiopia. Kihistoria wananchi wa Ethiopia hupenda kusema walitawaliwa na Malkia Sheba nyakati za biblia, jambo ambalo wana fahari kubwa nalo, hata hivyo ukweli ni kwamba Taifa hilo lina jamii iliyogubikwa kwa mfumo dume.

Mabadiliko yanayofanywa na Abiy Ahmed tangu alipoingia madarakani yameonyesha dalili zote za kuinua nafasi ya mwanamke na kumfanya kiongozi mwenye ushupavu na uwezo wa kuongoza katika nafasi mbalimbali.

Takwimu zilizokusanywa na Serikali ya Ethiopia na taasisi nyingine zinaonyesha kuwa: takriban asilimia 25 ya wanawake hutegemea uamuzi wa waume zao. Karibu asilimia 50 ya wanawake wamewahi kunyanyaswa katika mahusiano na wapenzi wao. Chini ya asilimia 20 ya wasichana wanajiunga shule za sekondari.      Zaidi ya asilimia 40 ya wanawake wanaolewa kabla ya kutimiza miaka 18.

Waziri mkuu huyo ametekeleza mageuzi mengi tangu aingie madarakani Aprili mwaka huu. Taifa la Ethiopia linabadilika kwa kasi chini ya utawala wake, huku wanawake wakionekana sasa kushikilia nyadhifa kuu za uongozi katika nchi ambayo wamegubikwa zaidi katika majukumu ya kitamaduni.

Wanawake ambao ni nusu ya idadi kamili ya milioni 102.5 ya watu nchini humo, wana majukumu ya kitamaduni zaidi, hususan maeneo ya mashambani, muda wao mwingi huwa nyumbani, wakilea watoto, kutafuta kuni au kuteka maji mitoni na kulima.

Ifuatayo ni orodha ya wanawake walioteuliwa kushika nyadhifa za juu nchini Ethiopia.

BIRTUKAN MIDEKSA

Huyu ameteuliwa karibuni kuwa Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Ethiopia. Amewahi kuwa Jaji na kiongozi wa chama cha upinzani cha Unity for Democracy and Justice (UDJ) cha nchini Ethiopia kuanzia mwaka 2008 hadi 2010. Sasa ameapishwa kuiongoza Tume hiyo.

Uteuzi wa Birtukan Mideksa ni muhimu kwa wanawake waliochaguliwa kufikia sasa kushikilia nyadhifa kuu serikali.

Birtukan alirudi Ethiopia mwezi huu baada ya kuishi uhamishoni nchini Marekani kwa miaka 7. Yeye ni miongoni mwa viongozi wa upinzani waliofungwa baada ya uchaguzi uliozusha mzozo mwaka 2005 uliochangia vifo vya mamia ya watu.

Baada ya uteuzi wake, Birtukan amesema anahisi taaluma yake ya ujaji itamsaidia kutatua mizozo na tofuati ambazo huenda zikazuka katika wadhifa wake mpya. Lakini ameongeza kuwa wananchi nchini kote wamedhihirisha kwamba wapo tayari kwa mageuzi.

“Raia wa Ethiopia wako tayari kujenga mfumo wa demokrasia wanaoutaka na kuiwajibisha serikali na wamelidhihirisha hilo kwa kujitolea ipasavyo. Kwahivyo naamini utayari wa umma ni nafasi moja nzuri mno,” amesema Birtukan katika mkutano wake na vyombo vya habari baada ya kuteuliwa.

Birtukan anakabiliwa na changamoto katika kurudisha imani katika Tume ya uchaguzi ambayo mara kwa mara imekabiliwa na shutuma za kuendeshwa na serikali  na atasimamia uchaguzi Mei mwaka 2020.

Kihistoria Birtukan alizaliwa mwaka 1974 mjini Addis Ababa. Alisoma sekondari ya Etege Menen na baadaye kujiunga Chuo Kikuu cha Addis Ababa  na kuhitimu shahada ya sheria. Mwaka 2014 alitunukiwa shahada ya uzamili ya utawala kutoka Taasisi ya WEB Du Bois ya Chuo Kikuu cha Havard.

MEAZA ASHENAFI

Novemba 18, mwaka huu mwanamama huyu aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani nchini Ethiopia. Amewahi kuwa wakili wa kutetea haki za binadamu, ambaye jitihada zake za kukabiliana na ndoa za utotoni ziliigizwa kwenye filamu ya muigizaji mashuhuri wa Hollywood nchini Marekani, Angelina Jolie 2014.

Meaza Ashenafi alizaliwa mwaka 1964 katika Kijiji cha Asosa, Benishangul-Gumuz nchini Ethiopia. Ni Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria wanawake (EWLA) ambacho kilianzishwa mwaka 1995.

Kati ya mwaka 1989 na 1992 alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Ethiopia. Mwaka 1993 aliteuliwa na Tume ya Katiba ya Ethiopia kuwa mshauri wao wa kisheria.

Vilevile Ashenafi amewahi kushikilia wadhifa wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa barani Afrika. Ni miongoni mwa waanzilishi wa Benki ya Wanawake ya Enat iliyoanzishwa mwaka 2011 na mwaka 2016 akawa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi.

BILLENE ASTER SEYOUM

Billene ni mtaalamu wa mawasiliano ambaye ameteuliwa kuwa msemaji wa kiongozi wa nchi hiyo. Billene Seyoum Woldeyes ana shahada ya uzamili katika masuala ya jinsia na amani aliyopata katika Chuo Kikuu cha Amani nchini Costa Rica. Pia shahada nyingine ya uzamili katika amani, ulinzi, maendeleo na utatuzi wa migogoro ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Innsbruck cha nchini Austria. Awali alipata shahada ya kwanza ya mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha British Columbia cha mjini Vancouver huko Canada

SAHLE-WORK ZEWDE

Hivi karibuni wabunge nchini Ethiopia walimchagua Sahle-Work Zewde kuwa Rais wa kwanza mwanamke Ethiopia. Sahle-Work ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu ambaye sasa amekuwa kiongozi wa kipekee mkuu mwanamke barani Afrika.

Kuchaguliwa kwake katika wadhifa huo kunajiri baada ya Abiy Ahmed kuliteua baraza la mawaziri, nusu ya nyadhifa katika baraza hilo zimewaangukia wanawake.

Katika hotuba yake ya kukubali wadhifa huo, Rais Sahle-Work alizungumza kuhusu umuhimu wa kudumisha amani, vyombo vya habari nchini vinaeleza. Alichaguliwa baada ya kujiuzulu ghafla kwa kiongozi aliyekuwepo Mulatu Teshome.

Mkuu wa wafanyakazi katika ofisi ya waziri mkuu, Fitsum Arega, alituma ujumbe katika mtandao wa twitter kwamba uteuzi huo wa “Kiongozi mkuu mwanamke haidhihirishi viwango vya miaka ijayo, lakini pia inafanya kuwa jambo la kawaida kwa wanawake kuwa waamuzi wakuu katika maisha ya umma”.

Sahle Work Zewde  amewahi kuwa Balozi wa Ethiopia nchini Senegal na Djibouti. Ameshikilia nyadhifa kadhaa katika Umoja wa Mataifa, ikiwemo mkuu wa kujenga amani katika Jamhuri ya Afrika ya kati.

Kabla ya kuwa Rais wa Ethiopia, Sahle-Work alikuwa mwakilishi wa UN katika Umoja wa Afrika. Kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia, rais hana nguvu ikilinganishwa na wadhifa wa waziri mkuu ambaye mwenye nguvu za kisiasa nchini.

Taswira iliyopo imeibua swali kuwa hatua hiyo ni nuru ya Ethiopia?

Swali hilo linaulizwa katika duru za kisiasa kutokana na uzoefu uliopo nchini humo wa siasa za mabavu huku maelfu ya wananchi wanaounga mkono upinzani na viongozi wao wamekuwa wakitupwa jela.

Duru za kisiasa zinapambanua kuwa kwa taswira hiyo, uamuzi wa Abiy Ahmed kuwainua wanawake katika nyadhifa kuu umekaribishwa na wengi, huku makundi ya kutetea haki za binaadamu yakitumai kuwa serikali mpya italiendeleza hili zaidi kwa kuzindua miradi mikubwa katika miezi ijayo kuimarisha maisha ya wanawake wa kawaida.

Abiy, mwenye umri wa miaka 42, amewapa wanawake nusu ya nyadhifa za uwaziri katika serikali kwa viti 20. Tofauti na viti 4 vilivyoshikiliwa na wanawake katika baraza kubwa zaidi la kiongozi aliyekuwepo Hailemariam Dessalegn. Ethiopia na Rwanda ndiyo sasa mataifa pekee ya Afrika yalio ana idadi sawa ya uwakilishi wa kijinsia katika baraza la mawaziri.

Uwepo wa wanawake hawa katika uongozi unatarajiwa kumsaidia Abiy anayetoka katika jamii kubwa ya Oromo nchini humo. Abiy amezaliwa na baba Muislamu huku mama akiwa Mkristo.

Kulifikia si tu suala la usawa wa kijinsia, lakini pia kupanua uungwaji mkono wake miongoni mwa makundi ya wachache na Waislamu ambao mara kadhaa hulalamika kutengwa kisiasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles