27.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

WANAWAKE CHADEMA KUULA 2020

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vicent Mashinji, amesema uchaguzi ujao wanawake watapewa nafasi kubwa ya kuwakilisha majimboni kutokana na ushindi waliouonyesha Uchaguzi Mkuu uliopita.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha).

Alisema katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015, wanawake waliopewa nafasi majimboni kuwania ubunge na uwakilishi walikuwa tisa ambao walionyesha uwezo mkubwa na kufanikiwa kushinda viti sita.

“Hiyo ni dalili tosha kuwa wanawake ni jeshi kubwa na hata kama wangepewa wengi nchi nzima, walikuwa na uwezo wa kufanya vizuri zaidi,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema taswira ya chama hicho mitaani ni kwamba kinaongozwa na nguvu kubwa na hivyo kuwekwa katika nafasi ya kuonekana ni cha wanaume pekee jambo ambalo si kweli, hivyo ni vyema kuongeza idadi ya wanawake katika uwakilishi majimboni.

Dk. Mashinji alisema anaamini wanawake watakaopewa nafasi za kuwakilisha majimbo, watafanya vizuri kwani sio wa kuingia kwa ajili ya kuuza sura bali ni jeshi la ushindi.

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Dk. Mashinji alisema Serikali ya CCM ina lengo la kuzorotesha wapinzani, lakini  pamoja na hali hiyo watakwenda nao sambamba huku wakitumia mbinu ili kuweza kushinda zaidi.

“Pamoja na jitihada za kuizorotesha Chadema na upinzani kwa ujumla kama wanavyofanya wateule wa rais, wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya kwa kuwakamata watendaji wa ngazi za chini, kutangaza kuwanyang’anya mihuri ya kazi, lakini bado kuna nguvu ya kuendelea kuimarisha chama.

“Viongozi wa chini wananyanyaswa, wanapigwa na viongozi wateule wa rais pasipo sababu na mfano mzuri Iringa, na hata ‘muvi’ ya mihuri ilitengenezwa ili kuwakomoa Ukawa,’’ alisema Dk. Mashinji.

Alizungumzia pia Ukawa inavyopambana katika chaguzi ndogo kutokana na CCM kuelezwa kutumia nguvu kubwa ya vyombo vya dola ya kuwakandamiza wapinzani, huku akitolea mfano uchaguzi mdogo wa ubunge Dimani na Igunga.

Dk. Mashinji alisema matatizo hayo yatakwisha endapo kutakuwa na Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, alisema wanawake wa Chadema walikuwa na nguvu katika uchaguzi uliopita kutokana na matokeo yake.

Alisema katika ubunge licha ya kupewa nafasi chache za kuwakilisha majimbo, lakini walifanya vizuri huku akiyaelezea majimbo mawili yaliyokuwa na mfumo dume lakini wamefanikiwa.

Alisema ishindi wa Esther Bulaya Bunda Mjini na Esther Matiko Tarime Mjini ni ishara tosha kwamba wanawake ni jeshi kubwa na linaweza kuongoza na kusimama jimboni na kushinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles