30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

RIDHIWANI AIBUKA SAKATA LA DAWA ZA KULEVYA

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), amesema suala la mapambano ya dawa za kulevya liachiwe Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya chini ya utendaji kazi wa Kamishna Mkuu, Rogers Sianga, aliyeteuliwa na Rais Dk. John Magufuli hivi karibuni.

Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alitoa kauli hiyo jana katika kipindi cha ‘East Africa Breakfast’ kinachorushwa na Kituo cha East Africa Radio kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 3 asubuhi.

Alisema anafikiri vita hiyo ni jambo jema kwani kwa mtu ambaye mambo hayo hayajamkuta, hawezi kuelewa madhara yake na kwamba nguvu kazi ya taifa imekuwa ikipotea kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya.

Ridhiwani alisema ni jambo la kupongezwa Serikali kwa jitihada zinazochukuliwa hivi sasa kutokana na jinsi tatizo hilo lilivyokuwa kubwa.

“Tumeshuhudia vijana wetu wengi wakipoteza uhai. Mfano, msanii wa muziki, Langa (Kileo) ambaye nilijaribu kumsaidia bila mafanikio. Hata kule kwetu vijana wengi wamepoteza maisha, hivyo vita hii kamwe haitakiwi kushindwa, tupo pamoja na Serikali yangu kuhakikisha kuwa tunaifikisha mwisho vita hii.

“Kwani vita hii ni vita pana ambayo inatakiwa kuwa kwenye sera yetu na tayari rais amemteua Kamishna Mkuu, Sianga ambaye ni  ‘very  capable man’, ni mtu mwenye uwezo mkubwa, hivyo atafanya kazi vizuri.

“Ninachowaomba Watanzania tumpe ushirikiano kwani tayari tumeona amekabidhiwa majina ya watu 97 ambapo tunaamini watakaobainika watashughulikiwa.

 “Hii ni vita kubwa sana, hivyo niipongeze Serikali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwani naamini kwa mahala tulipofikia tutafanikiwa kwani Sianga amepata elimu ya dawa za kulevya nchini Ujerumani na kupata mafunzo makubwa, yakiwamo yale ya kutumia mbwa, hivyo kazi hii tumwachie,” alisema mbunge huyo na kuongeza.

 “Unakumbuka kipindi kile msanii Ray C (Rehema Chalamila) alikuwa anaamka saa 9 usiku kwenda kutafuta dawa ili tu akae vizuri hadi anapiga kelele kwamba ‘wananibaka’, hivyo ni janga kubwa,” alisema.

Akifafanua zaidi, alisema taarifa ambazo zimekuwa zikimuhusisha na utajiri zinatolewa na watu ambao hawamjui vizuri.

“Unajua bahati mbaya sana iliyopo kwenye maisha tunayoishi, ni kwamba watu wanaishi kwa dhana, kuna mahala ukienda unakuta watu wanakujadili ili tu ujue hivyo, wengi wao ni dhana ambayo wamejiwekea.

“Mengi yanasemwa sana lakini napenda wafahamu kuwa tunaishi kawaida kulingana na kipato cha jasho letu, lakini kwa watu ambao hawanifahamu unakuta ndio wanasema kuwa mimi ni tajiri mara namiliki vituo vya mafuta na majengo, hapana,” alisema.

Aliongeza kuwa binafsi anaamini katika kufanikiwa lazima uache alama na kwamba hata yeye anatamani kuacha alama hizo na kusisitiza kuwa wengi wa wanaomnyooshea kidole kuwa ni tajiri hawamjui.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo alisema kuwa amefikia mafanikio ya kisiasa kutokana na jitihada zake na si kwa mgongo wa baba yake.

“Mimi nilianza siasa nikiwa na umri wa miaka mitano mwaka 1984, ambapo babu yangu ndiye aliniingiza kwenye siasa hadi kunikutanisha na Mwalimu Julius Nyerere aliyenisisitiza kukua vizuri kama baba yangu, hivyo nimejengwa na kupitia hatua zote anazopaswa kupitia mwanasiasa, hivyo naweza kusema kwamba mimi ni zao la kijana aliyetengenezwa, hivyo sikupata ubunge kwa kigezo cha kuwa mtoto wa rais,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles