Masyenene Damian, Misungwi
Baadhi ya wanaume katika Kijiji cha Mwanangwa Kata ya Mabuki wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, wamedai mifarakano baina ya wanandoa, usaliti na umaskini wilayani humo inatokana na wanawake kuuza mavuno ya mazao kinyemela ili kununua vipodozi.
Madai hayo yamekuja siku chache baada ya wanawake kudai kutelekezwa na waume zao nyakati za mavuno kutokana na kuchukua fedha za mauzo ya mazao mbalimbali kisha kwenda kutumia na wanawake wanaofanya ukahaba kutoka Jijini Mwanza ambao wamepewa jina la ‘Nzige’.
Wakizungumza juzi kwenye mdahalo maalumu wa kujadili namna ambavyo kipindi cha mavuno kinakuwa na changamoto wilayani humo, ulioandaliwa na Shirika la Kutetea haki za Wanawake na Watoto la Kivulini, wamesema migogoro mingi huzuka wakati wa mavuno.
Mmoja wa wanaume waliochangia kwenye mdahalo huo, Mussa Kiyumbi, amesema chanzo cha migogoro na hata kupigwa kwa wanawake katika ndoa, kimekuwa kikitokana na wao kuwanyima unyumba lakini pia huuza mazao kinyemela ya familia kinyemela.
“Wanawake hawa wanauza mazao kinyemela kwa lengo la kwenda kununua vipodozi ambavyo waume zao hawavijui, wanabeba mazao kidogo kidogo kwenye ndoo na kwenda kisimani kama wanaofuata maji, changamoto nyingine tukidai haki zetu za ndoa wake zetu hawaridhii ndiyo maana tunatoka nje kutafuta suluhu na kupoza hasira kwa Nzige,” amesema.
Mmoja wa wanawake wilayani hapo, Regina Kubunga, amesema wanawake wengi wamekuwa wakiamua kuuza mavuno ya mazao ya akiba kwenye nyumba zao ili kumudu gharama mbalimbali kutokana na wanaume kuuza na kumalizia fedha zote kwenye anasa na ulevi.
“Unakuta nyumbani hamna hata bustani ya mboga, hufugi kuku sasa wanapokuja wageni baba hayupo, inabidi uhangaike hayo ndiyo matokeo yake wanawake nao huchukua kwenda kuuza sehemu ya mazao ili wapate fedha za kutatulia matatizo, hivyo sababu ni wanaume kushindwa kutimiza wajibu wao wa kutunza familia,” amesema.