25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasiasa wahofia mfumo wa BVR

Jaji Damian Lubuva
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva

Na Grace Shitundu, Dar es Salaam

BAADHI ya wanasiasa wameonyesha wasiwasi wao kutokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanzisha mfumo mpya Biometric Voter Registration (BVR) wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura ambao unatarajiwa kuanza Septemba mwaka huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, wanasiasa hao walisema kuwa mfumo huo ni mpya kutumika hapa nchini lakini pia umetambulishwa kwa kipindi kifupi wakati kuna changamoto zake.

“BVR ni mfumo mpya ambao unaanza kutumika hapa nchini, licha ya Zanzibar kuutumia tangu mwaka 2009, lakini wananchi wa Tanzania Bara bado hawaujui.

“Katika mfumo huu kuna baadhi ya nchi zimefanikiwa na nyingine hazikufanikiwa, hii inatokana na kujitokeza kwa changamoto ambazo zimesababisha wananchi kulalamika,” alisema Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.

Alisema makada wa CCM wana maswali mengi ya kuwauliza watu wa NEC kutokana na kuanzisha mfumo huu, ili tuweze kuuelewa kabla ya kwenda kwa wananchi kuwahamasisha wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari hilo.

Alisema mfumo wowote mpya haukosi changamoto zake hivyo basi, NEC inapaswa kujifunza changamoto hizo ili waweze kuzifanyia marekebisho kabla ya kuanza kutumika hali ambayo inaweza kuepusha malalamiko.

Kinana alisema kuwa, Serikali inatumia gharama kubwa kuandaa vitambulisho tofauti ambapo kungekuwa na utaratibu wa kuandaa vitambulisho vya aina moja ambavyo vingeweza kutumika kwenye maeneo tofauti.

Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali ilipaswa kuangalia mfumo mmoja wa utengenezaji wa vitambulisho hivyo ili viweze kutumika kwenye shughuli mbalimbali za kitaifa kama vile upigaji kura na utambulisho.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa hawana imani na mfumo huo kwa sababu umeletwa muda mfupi wakati wananchi wanajiandaa na Uchaguzi Mkuu mwakani.

“Hatuna imani na utendaji wa NEC kwa sababu wameshindwa kutumia kampuni iliyosambaza mashine hizo mpaka sasa ili zije kutumika kwenye uboreshaji wa daftari la wapiga kura.

“Ukiangalia muda uliobaki ni mfupi sana kuelekea Uchaguzi Mkuu, hivyo basi tunaamini hawawezi kuandikisha wapiga kura katika kipindi hiki kifupi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema mwaka 2010, NEC waliwaita kwa ajili ya kuzungumzia uboreshaji wa daftari hilo na kuwaambia kuwa vitambulisho vya zamani vilikuwa bora na kwamba vinafaa kutumika kwenye chaguzi mbalimbali zijazo.

Alisema lakini mwaka huu wamekuja na kauli nyingine ya kuwaambia mfumo huo haufai, unasababisha kupoteza taarifa za wapiga kura, hali iliyowafanya watumie mfumo mpya wa BVR.

Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alisema kuwa hawana imani na mfumo huo kwa sababu wameambiwa katika muda mfupi.

“Wametuita kujadili suala hili wakati muda uliobaki ni mfupi, kama walikuwa wanataka kufanya maboresho kwanini wasingefanya mapema ili tuweze kuutafakari kwa kina na kutoa ushauri wetu wa nini kifanyike ili kuboresha daftari hili,” alisema Lissu.

Aliongeza kwamba, suala si kubadili mfumo bali ni kubadili sheria ambayo inampa mwananchi nafasi ya kupiga kura hata kama amepoteza kitambulisho ikiwa taarifa zake zitakuwa zimehifadhiwa kwenye kanzi data ya wapiga kura.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, alisema lengo la kutumia mfumo huo ni kuboresha daftari la wapiga kura na kuondoa changamoto zilizojitokeza wakati wa utumiaji wa mfumo wa zamani wa Optical Mark Recognition (OMR).

Alisema katika mfumo huu wa OMR, baadhi ya taarifa za wapiga kura zilipotea kutokana na kushindwa kuhifadhiwa kwenye kanzi data, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kushindwa kupiga kura kwenye chaguzi zilizopita.

Alisema kutokana na hali hiyo, NEC imeamua kutumia mfumo huu wa BVR ili kutoa nafasi ya uhifadhi wa taarifa sahihi za mpiga kura.

Hoja kuhusu suala la mashine za BVR ililiibuliwa mwaka jana na mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (Chadema), ambaye aliitaka Serikali kufanya uchunguzi kuhusu upatikaji wa kampuni iliyopewa tenda ya mashine hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles