27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mgeja ataka Mangu, Mwamunyange wakomeshe ugaidi

IGP Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu

NA SITTA TUMMA, MWANZA

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, amemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu pamoja na Mkuu wa Majeshi, Jenerali David Mwamunyange, kuweka mikakati maalumu ya kudhibiti matukio ya kigaidi na uhalifu wa kutumia silaha hapa nchini.

Amesema hivi sasa amani ya Tanzania inaonekana kuanza kutikiswa kutokana na kuwepo kwa matukio ya kigaidi katika baadhi ya mikoa na maeneo mengine, hivyo IGP Mangu na Jenerali Mwamunyange ni vema wakajipanga kukabiliana na uhalifu huo haramu.

Mgeja alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza, muda mfupi baada ya kumjulia hali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Mkoa wa Shinyanga, Juma Kimisha, aliyelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), jijini hapa baada ya kutekwa na kupigwa risasi na majambazi.

Mgeja alisema milipuko ya mabomu na uharamia wa kutumia silaha nzito za kivita unaosababisha vifo, majeruhi na vilema vya kudumu, vimeonekana kukithiri hivyo kuanza kuiweka rehani amani, upendo na utulivu ulioachwa na Baba wa Taifa, hayati Julius Kambarage Nyerere.

“Amani ya nchi yetu kwa sasa imeanza kujaribiwa na maharamia na ili tudhibiti ugaidi huu, IGP Mangu na Jenerali Mwamunyange ni vema wakajipanga sawasawa kuikabili hali hii ya hatari katika taifa letu.

“Milipuko ya mabomu na matukio mengine ya silaha nzito za kivita lazima yakomeshwe. Naomba kila mwananchi avunje ukimya kwa kushirikiana na Serikali kufichua wahalifu maana wanaishi ndani ya jamii yetu na hii itakuwa ni faida ya taifa na maendeleo ya kila mtu,” alisema Mgeja.

Mwanasiasa huyo alilaani tukio hilo la kushambuliwa kwa risasi Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu na aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Polisi Jamii zilizopo kwenye maeneo yao ili kuweza kupambana na uhalifu wa aina yote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Kimisha aliwaambia waandishi wa habari walioongozana na msafara wa Mwenyekiti Mgeja kwamba, aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza nguvu ya kupambana na kudhibiti uhalifu kwani unarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Alisema tukio hilo lilitokea Julai 2 mwaka huu 2014, wakati wakitoka kwenye maonyesho ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Tanga kwa gari aina ya Toyota Prado, SM 10023 mali ya Halmashauri ya Ushetu, wakakuta kizuizi cha mawe barabarani kati ya majira ya saa 2:30 usiku.

Naye daktari bingwa wa masuala ya upasuaji wa moyo na kifua katika Hospitali hiyo ya Bugando, Dk. Godwin Sharau, alisema risasi iliyokwama mwilini haina madhara kwa sababu ipo pembeni mwa uti wa mgongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles