Mwandishi Wetu na Mashirika ya Habari |
IMEBAINIKA kuwapo aina tano za ugonjwa wa kisukari, miongoni mwake zikiwamo zile ambazo zilikuwa hazitambuliki vema kwa madaktari na wagonjwa wao.
Utafiti mpya uliofanywa na taasisi ya Lancet Diabetes & Endocrinology ya nchini Finland na Sweden, umeonyesha aina tano ambazo zinaweza kupatiwa matibabu tofauti kulingana na muundo wake.
Aina hizo ni pamoja na ‘Autoimmune diabetes’ ambayo inamshambulia mtu tangu akiwa kijana na kuathiri uzalishaji wa ‘Insulin’.
Nyingine ni ‘Severe Insulin-deficient diabetes’ (SIDD), ambayo mgonjwa huonekana kama ameathiriwa na aina ya kwanza, huwa na uzito mkubwa na mwili huhangaika kuzalisha ‘Insulin’ na kuathirika mfumo wa seli, tishu na ogani za mwili.
Aina ya tatu ni ‘Severe Insulin-Resistant Diabetes’ (SIRD), ambayo huonekana kwa mgonjwa ambaye ana uzito mkubwa sana na kuzalisha ‘Insulin’.
‘Mild obesity-related diabetes’ (MOD) ni aina nyingine ambayo hutokea mwanzoni kwa watu wanaougua ugonjwa wa kisukari, hasa wakiwa na uzito mkubwa na kitambi, lakini mfumo wa mabadiliko unakuwa si wa kawaida kama aina ya tatu.
Aina ya tano ni ‘Mild Age-related diabetes’ ambayo mgonjwa anaonyesha dalili wakati akiwa na umri mkubwa na kuonyesha hisia fulani dhidi ya wengine, hasa kitabia.
Wanasema aina hizo ni ngumu kupatiwa dawa mahususi ili kutokomezwa.
Watafiti wanasema kuwa aina hizo za kisukari zinaweza kuleta usumbufu miaka ijayo na mabadiliko ya tiba huenda yasipatikane haraka.
Kisukari kinaathiri mtu mmoja kati ya watu wazima 11 duniani kote na ongezeko la hatari ya kupata magonjwa ya shinikizo la damu, kiharusi, upofu na figo.
Aina ambazo zilikuwa zikitambulika kabla ya utafiti huo mpya, ni diabetes type -1 ambayo mara nyingi huathiri mfumo wa kinga ya karibu asilimia 10 ya watu nchini Uingereza.
Mfumo wa kinga kupitia Insulin unashambuliwa na hakuna homoni za uhakika kudhibiti kiwango cha sukari.
Aina ya pili, ‘diabetes type -2’ inatokana na mfumo mbovu wa maisha, mfano uzito kupita kiasi unaweza kuathiri utendaji wa kazi wa Insulin.
Utafiti huo kutoka Idara ya Ugonjwa wa Kisukari ya Chuo Kikuu cha Lund nchini Sweden na Taasisi ya IMM ya Finland, ulihusisha wagonjwa 14,775 ambao walifanyiwa vipimo vya damu zao.
Utafiti huo unatajwa kuwa msaada mkubwa kwa madaktari na wagonjwa ili kukabiliana na ugonjwa hatari wa kisukari.
Inaelezwa ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa magonjwa yatokanayo na utendaji kazi wa mwili.
Ili mwili ufanye kazi zake vyema, lazima upate sukari (glucose) na kuitumia ili kutengeneza nishati.
Wataalamu wanasema kutokana na nishati hiyo, ubongo utafanya kazi yake vizuri, macho, mapafu na viungo vingine mwilini.
Sambamba na umuhimu huo wa sukari, bado haitakiwi kuzidi kwakuwa husababisha ugonjwa wa kisukari.
Ugonjwa wa kisukari ni kuzidi kwa sukari (glucose) ndani ya mishipa ya damu na hali hiyo inatajwa kuwaathiri watu milioni 420 duniani.