AJALI YAUA SITA DODOMA

0
1015

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Watu sita wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma baada ya lori la kubeba kokoto na gari la kuzoa taka la Manispaa ya Dodoma, kugongana uso kwa uso.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Dodoma Gilles Muroto amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Jumapili Machi 4, katika eneo la Changarawe Kata ya Ntyuka mkoani Dodoma.

“Ni kweli ajali hiyo imetokea katika maeneo hayo, na hali za majeruhi si nzuri wanatibiwa Hospitali ya Mkoa ambako wamekimbizwa,” amesema Muroto.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Carolina Damian pia amethibitisha kupokea miili sita katika ajali hiyo.

“Ni kweli hapa kwangu tumepokea miili ya vijana sita waliokuwa kwenye lori ambalo tunaambiwa lilifeli breki zake katika mtelemko wa Ntyuka, bado tunawasiliana na wenzetu zaidi,” amesema Dk. Carolina.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here