MOSCOW, URUSI
WANASAYANSI na viongozi wa kisiasa nchini Urusi wanadai Marekani ndiyo iliyotengeneza virusi vya corona vilivyoanzia katika jiji la Wuhan na kusabababisha maafa makubwa nchini China.
Wanaamini virusi hivyo ni silaha iliyotengenezwa kwenye maabara kwa ajili ya kuituliza China wakati wao wakitengeneza mabilioni ya faida kwenye kampuni za dawa za Marekani.
Urusi ilifunga mpaka wake na China kama njia ya kujikinga na kitisho cha virusi hivyo.
Mjadala kuhusu virusi hivyo na mtazamo kuhusu wanasayansi hao wa Urusi mbali na kuripotiwa na vyombo vingine vya habari lakini pia siku sita zilizopita uliripotiwa na shirika la habari la Marekani la CNN.
Vyanzo vya vyombo vya habari cha Urusi vinaamini kuwa virusi hivyo vimetengenezwa kuiangamiza China.
Hata hivyo katika mjadala huo uliochapishwa na CNN imeeleza kuwa madai hayo ambayo yamepewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari vya Urusi huenda ni juhusi cha Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin kudhoofisha maslahi ya Marekani nchini China.
Madai hayo yamekuja wakati ambapo idadi ya waliokufa kwa maambukizi ya virusi vikali vya Corona nchini China ikifikia 722 huku idadi ya waliombakuzwa nayo ikiongezeka kwa kasi na kupindukia hadi 34,500.
Mvutano wa hivi karibuni kati ya China na Marekani unajulikana.
Mgogoro huo unaonekana kama pambano kubwa kati ya taifa kubwa lililokuwa na nguvu ya kiuchumi na lile linaloibukia na hata kulitishia jingine.
Mgogoro ulikwenda mbali zaidi kutoka kwenye masuala ya biashara hadi bahari ya kusini ya China na mtandao wa intaneti wa 5G.
Baadhi nchini Urusi wanaamini mvutano huu umeishinikiza Serikali ya Marekani kuchukua hatua kali kufikia malengo yake.
Igor Nikulin, ambaye alikuwa Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Silaha za Biolojia na Kemikali, anadai kwamba aliwasiliana na wenzake wa China ambao wanaamini virusi vya corona vilitengenezwa na mwanadamu.
Nikulin anasema; “Yote inaonekana kama hujuma. Kwanza kabisa, huu ni mji wa Wuhan – ni kitovu cha nchi, kitovu kikuu cha usafirishaji, pamoja na sasa Mwaka Mpya wa China – mamia ya mamilioni ya Wachina watasafiri kuzunguka nchi kwa jamaa, marafiki, na kadhalika”.
Nikulin anaendelea kutoa maoni ya kushangaza zaidi (na labda dhahiri) – kwamba mashirika ya Marekani yanaweza kuwa yameunda virusi vya corona vya Wuhan kupata fedha kutokana na tiba.
Nikulin sio mtu pekee aliyekaririwa akisema hayo Wanasiasa pia hutumia fursa hiyo kuishambulia Marekani.
Vladimir Zhirinovsky, kiongozi wa LDPR nchini Urusi, ameweka wazi hadharani kwamba Marekani inaweza kusababisha mzozo huo kudhoofisha nguvu ya uchumi ya China wakati yenyewe ikitengeneza mchakato wa kupata fedha nyingi.
Alisema, wafamasia watakuwa mabilionea mwaka huu wa 2020 na kila mtu mara moja atasahau kila kitu.
Baadhi ya Wachina wamechukua mawazo hayo kwa makini lakini kwa mujibu wa Hu Xijin, mhariri wa Global Times nchini China anasema wengi hawaamini.
Ijumaa Rais Xi Jinping wa China alizungumza na Rais Donald Trump na kuitaka Marekani kushiriki haraka katika kukabiliana na mripuko wa virusi vya corona, na hasa kutokana na malalamiko ya baadhi ya nchi kuwazuia wasafiri kutoka China.
Hata hivyo Marekani imetanagaza kutumia dola milioni 100 kuisaidia China na Mataifa mengine kukabiliana na mripuko huo.
Tani 18 ya vifaa vimetolewa pia ikiwa msaada kutoka kwa watu wa Marekani.
Miongoni mwa hivyo vimo vya kujikinga na maambukizi na vinginevyo.
Lakini pamoja na hayo mamia ya Wamerekani wameondolewa katika maeneo hatarishi.
Katika kipindi cha mwaka 2002 na 2003, ugonjwa wenye kufanana na huu unaosababaishwa na corona uliopewa jina la SARS ulisababisha vifo vya watu 650 na hivyo virusi vya corona kutajwa kuwa ugonjwa unaotishia.