Asha Bani
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Tate Ole Nasha amesema serikali haitegemei kuona vitabu ambavyo havina ithibati ya serikali na ikigundulika hivyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Hayo yalielezwa leo wakati wa uzinduzi wa usambazaji vitabu vya kiada darasa la kwanza mpaka la tano kwa shule zinazotumia lugha ya kingereza na vile maandishi ya nukta nundu darasa la kwanza mpaka lanne na kidato cha 1 mpaka cha nne.
Ole Nasha amesema shule zote zitatumia vitabu vyenye ithibati ya serikali haijalishi shule ya medium au shule za serikali za kawaida.
“Shule zote zitumie vitabu vyenye ithibati ya serikali haijalishi wewe unatoka Atlas wala wapi.
“Ukionekana unapindisha maagizo hayo basi sheria itachukua mkondo wake na vitabu hivi hakikisheni vinapelekwa mashuleni haraka tayari kwa kutumiwa uwiano ulioelekezwa,”amesema Olenasha.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Aneth Komba yeye alikazia kauli ya waziri na kutoa wito kwa wamiliki wa shule binafsi, wazazi na wadau wengine wa elimu kutumia vitabu vya kiada na ziada vilivyopata idhini ya serikali.
“Niwaombe wasimamizi wa elimu wakiwemo wadhibiti ubora wa shule kusimama na kuhakikisha kuwa shule zinatumia vitabu sahihi na kwa idadi ya vitabu vilivyopo kwa sasa hakuna kabisa sababu ya kutumia vitabu ambavyo havina idhini ya serikali,” amesema Dk. Komba.