28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

WANAOPINGANA NA TRUMP WANAJIUZULU, WASIOKUBALIANA NA MAGUFULI VIPI?

Na M. M. Mwanakijiji,

BAADA ya Donald Trump kuchaguliwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, siyo watu wote ndani ya serikali yake na kwenye chama chake walikubaliana naye. Kuna ambao walimpinga kuanzia alipotaka kugombea na wengine walimpinga baada ya kuchaguliwa.

Ndani ya serikali yake kuna watu ambao waliikataa misimamo mbalimbali ya kiutendaji na kisera ya Trump kiasi kwamba hawakuwa tayari kufanya naye kazi.

Misimamo ya Trump ambayo imewakwaza wengi ni pamoja na ile inayohusiana na sera zake za uhamiaji, mazingira, ulinzi na usalama na hata mambo yanayohusiana na tabia yake ambayo baadhi ya watu wanaiona ni ya kibabe na yenye kutukuza mfumo dume.

Tangu Trump kuingia madarakani, wapo wafanyakazi na watendaji mbalimbali ambao waliamua kuachia kazi zao – wengine wakiwa wametumikia muda mrefu tu – ili kupinga kufanya kazi chini ya mtu ambaye hawamkubali kisera na kitabia. Nitatoa mifano michache tu ili kuthibitisha hoja yangu hii, ili kuwakumbusha wale wanaopingana na Magufuli ndani ya CCM katika harakati zake za kufanya mabadiliko.

Edward Price

Huyu ni msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa na Ofisa wa Shirika la Kijasusi la Marekani la CIA. Yeye alijiuzulu kupinga jinsi Trump alivyotoa nafasi kwa mshauri wake wa mikakati kuingia katika Baraza la Usalama na kuwaondoa baadhi ya majenerali.

Akiandika kwenye gazeti la Washington Post, Price anasema hakudhania kuwa angefikia uamuzi wa kutoka CIA, lakini sababu ya Trump aliamua kuachia ngazi. Hakuwa tayari kufanya kazi chini ya Rais ambaye anapuuzia taarifa za kiintelijensia zenye maslahi ya taifa.

Mustafa Ali

Ni ofisa katika Idara ya Mazingira ya Marekani (EPA), ambaye alitumikia idara hiyo kwa miaka 20, aliamua kujiuzulu wiki iliyopita kupinga mpango wa Trump kukata bajeti ya idara hiyo.

Chini ya Trump, bajeti yake ya mwaka huu kwa idara hiyo itakatwa kwa karibu asilimia 25, jambo ambalo Ali hakuwa tayari nalo na aliona amepingana mno kimtazamo na Rais wake na hivyo aliamua kujiuzulu.

Mifano hiyo miwili ni ya watu wa serikalini; wapo wengine wengi pia ambao watafuata mkondo huo wa kujiuzulu. Ndani ya chama chake vile vile wapo watu ambao walimkosoa Trump na hawakuwa tayari kuendelea naye ndani ya chama. Mifano miwili hapa inatosha kusisitiza hoja yangu.

Beth Fukumoto 

Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani kwenye Jimbo la Hawaii, aliamua kujiondoa ndani ya chama cha Republican kufuatia shinikizo la viongozi wa chama chake baada ya yeye mara kadhaa kumkosoa Rais Donald Trump.

Kwenye maandamano ya wanawake yaliyofanyika Januari 21 (siku moja tu tangu Trump aapishwe), Fukumoto alizungumza kwenye maandamano hayo na kumuita Trump mbabe. Chama chake kilijaribu kumuasa, lakini hakuwa tayari kunyamaza na hivyo kuamua kuhama meli kumkimbia rais huyo mpya.

George Willis 

Miongoni mwa wa sauti za wahafidhina wa Marekani ambaye alikuwa maarufu sana na kwa muda mrefu akiandika makala mbalimbali za kisiasa. Mshindi wa tuzo ya Pulitzer na mwandishi wa muda mrefu, aliamua kuachana na chama cha Republican. Trump mwenyewe aliandika kwenye mtandao wa Twitter kupuuzia kujiondoa kwa George Willis.

Mifano hii ya aina mbili inanirudisha kwenye kichwa cha habari cha makala haya ya leo. Kuna watumishi na watendaji ndani ya Serikali ya Rais Magufuli ambao hawakubaliani naye. Vilevile wapo watendaji wengine ndani ya CCM hawakubaliani naye – ama kifalsafa au kiutendaji, au hata kiitikadi, lakini bado wanataka kuendelea kuwa watumishi. Vilevile ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Nadhani huu ni wakati wao wa kujiuzulu na kuachana na Serikali ya Magufuli au CCM pia, maana wanasigana katika mambo ambayo yanasababisha hasara kwa taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles