30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

MADABIDA CHOTA HEKIMA ZA SOFIA SIMBA

Na TOBIAS NSUNGWE,

NI mtikisiko! Ndivyo unavyoweza kuyaelezea mabadiliko yaliyofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wiki iliyopita mjini Dodoma.

Mabadiliko hayo yamewaacha makada wengi wa chama hicho bila vyeo, huku majina makubwa kabisa yakivuliwa uanachama wa chama hicho kikongwe kilichoasisiwa Februari 5, 1977.

Sofia Simba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT), ameondoshwa katika safu ya wakongwe ndani ya CCM. Bila shaka haikuwa jambo rahisi kufikia uamuzi huo.

Licha ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana kudai kuwa mabadiliko hayo yana lengo la kuongeza ufanisi na kukiimarisha chama hicho, hata hivyo, ukitazama kwa kina mabadiliko ya 16 ya Katiba ya chama hicho ni kama CCM kimezaliwa upya.

Katika tukio hilo, ni wazi kuwa si kila mwana CCM ameyafurahia mabadiliko yanayofanywa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli.

Kwanini baadhi hawayapendi mabadiliko hayo? Ni kwa sababu sasa, Mkutano Mkuu utahudhuriwa na wajumbe 163 badala ya 388. Hii ina maana wajumbe 225 wamefyekwa na hivyo kukosa fursa ya kupata posho na marupurupu mengine yanayoambatana na vikao hivyo, ikiwa ni pamoja na kujenga ‘mitandao’.  Kamati Kuu (CC) itabakiwa na wajumbe 24 badala ya 32.

Hivyo wajumbe nane wamefyekwa na kupunguziwa hadhi ya kuwa na ushawishi ndani ya chama.  Ingawa Rais Magufuli amesema ‘hatowatupa’ wale wote walioathiriwa na mabadiliko ya kupunguza wajumbe wa vikao vya chama, binafsi siioni nafasi ya juu ambayo mwanachama anaweza kuwa na ushawishi na kutamba kama akiwa ndani ya CC.

Nani atafurahia uamuzi huo ambao umewapoka baadhi wajumbe chanzo cha kupata ‘ulaji’? Wale waliokuwa wanaitegemea CCM kama chanzo cha mapato itawabidi wajipange upya, kwani kazi za chama sasa zinataka nidhamu zaidi, mapenzi ya dhati na moyo wa kujitolea. 

CCM imefanya uamuzi wa busara kupunguza utitiri wa vyeo kwa mtu mmoja. Haiwezekani mtu huyohuyo mbunge, mjumbe wa NEC, mjumbe wa CC na au waziri.

Kwa nyakati tofauti, Rais Magufuli na Kinana walielezea matumaini yao kwamba mabadiliko hayo yatarudisha nidhamu ndani ya chama.

Katika kile kinachoelezwa kukerwa na baadhi ya vitendo ndani ya chama hicho, Mwenyekiti wa CCM alikumbushia kitendo walichofanya wajumbe wa NEC mwaka juzi cha kuimba wimbo wa kumuunga mkono Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, wakidai kuwa wana imani naye.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kitendo kile kilikuwa ni ukosefu mkubwa wa nidhamu mbele ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa nchi, Jakaya Kikwete.  

Rais Magufuli amepata kunukuliwa akisema kama siku ile yeye angelikuwa Rais na mwenyekiti wa chama hicho, basi nusu ya wajumbe wale ‘wangekwenda’.

Magufuli alisema wale wote walioimba kuwa na imani na Lowassa hata baada ya chama kutompitisha ni ‘watu wa ovyo’ na akawashangaa baadhi ya makatibu waliokisaliti chama wakati ule, huku wakijua kuwa wao ni waajiriwa wanaolipwa mshahara na chama. Ujumbe wa mwenyekiti ni kwamba, hataki hali kama ile irudie.

Magufuli, aliyekuja na kaulimbiu ya CCM mpya Tanzania mpya, amewaonya wanachama na makada wa chama hicho wenye tabia ya kutumia rushwa kupata uongozi, ameapa kutopitisha mtu yeyote atakayethibitika kuwa katoa rushwa.

Mkutano huo maalumu umeshuhudia makada maarufu wa chama hicho wakifukuzwa chamani. Baadhi yao ni aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, ambaye inadaiwa alionekana waziwazi kuunga mkono upinzani wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mwingine ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, ambaye mbali ya kusababisha chama kushindwa vibaya mkoani kwake, pia anadaiwa kumfananisha Lowassa na Mtume! Pengine jina maarufu zaidi katika wale waliovuliwa uanachama ni Sofia Simba, aliyekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT).

Mengi yamezungumzwa kuhusu Sofia Simba, mwanasiasa mkongwe nchini, kubwa lililonifurahisha ni uamuzi wake wa kukataa kujiingiza kwenye malumbano na chama hicho.

Badala yake, amesema sasa anajiunga na kundi kubwa la wakereketwa wa CCM. Kuvuliwa uanachama hakumnyimi mtu fursa ya kuonyesha mapenzi yake kwa chama kwa namna nyingine.

Nasema Waziri huyo wa zamani amechukua uamuzi wa busara. Ni bora azipuuze kelele zinazomshawishi ajiunge kwenye upinzani. Sofia amejijengea heshima kubwa ndani ya CCM tangu alipojiunga mwaka 1971. Amepanda ngazi akiwa CCM. Amezoa marafiki akiwa CCM na kama alivyosema mwenyewe, amekuwa na bahati ya kufanya kazi na marais watatu.

Amekulia CCM. Ni vyema pia watu kama kina Madabida wakatulia. Si busara kwa watu kama Sofia Simba kutimkia upinzani. Iko hatari kwa makada wakubwa kujishushia heshima yao kama wakiamua kwenda upinzani, kwani wataishia kuitwa ‘makapi’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles