20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaopeleka wazazi makao ya wazee waonywa

OSCAR ASSENGTANGA

VIJANA wanaowapeleka wazazi wao nyumba za kulea wazee wasiojiweza maeneo mbalimbali nchini, wametakiwa kujiandaa kwenda kukaa huko wakiwa na umri wa utu uzima.

Wito huo ulitolewa juzi na Mratibu wa Taasisi ya Jamii ya Akhlaki Islamic Taifa (Jai), Dk. Salim Khalani, wakati walipotembelea wazee wanaolelewa Kituo cha Kulea Wazee cha Mwanzange jijini Tanga, katika kusherehekea Sikukuu ya Eid el-Hajj pamoja na kushiriki chakula cha pamoja.

Taasisi hiyo inayohudumia wagonjwa hospitalini na kufanya kazi za kijamii iliwatembelea wazee wa kituo hicho kuwafariji kwa kula nao chakula cha mchana.

 “Niwaambie kwamba vijana wote ambao wamewachukua wazazi wao na kuwaleta kwenye vituo vya kulea wazee wasione kama wamewafanyia hisani, bali watambue kwamba watoto wao watakuja kuwalipizia nao watakapofikisha umri kama wazazi hawa.

“Kila anayemfanyia baya mzazi wake malipo yake huwa ni hapa duniani,” alisema.

Dk. Khalani alisema kuna jambo mbalo ni lazima jamii itambue kwamba hata nyumba wanazolelewa wazee hao zimechakaa na zinahitaji ukarabati.

Awali akizungumza mara baada ya chakula cha pamoja, Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Juma Luwuchu, aliishukuru Taasisi ya Jai kwa kutambua wajibu wa kuwasaidia wazee hao na akaziomba taasisi nyingine zenye uwezo zisaidie vituo hivyo.

“Tuna kila nafasi ya kuwasaidia wazee wasiojiweza, niwashukuru Taasisi ya Jai, Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, taasisi hii niwashukuru.

“Tulivyonavyo tuvitoe kwa wazee ambao hawana watu wa kuwasaidia, lakini pia misaada hii isikome, itolewe kwa nyakati zote,” alisema Sheikh Luwuchu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles