23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wafugaji wapewa darasa malisho ya mifugo

JANETH MUSHI-ARUSHA

WAFUGAJI nchini wametakiwa kulima kwa wingi mazao ya malisho ya mifugo kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, ambayo yanachangia upungufu wa malisho hayo.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo  na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Felix Nandonde, wakati wa mdahalo ulioshirikisha wadau mbalimbali wa mifugo waliojadiliana changamoto, fursa na mafanikio yaliyopo katika sekta ya maziwa.

Dk. Nandonde alisema iwapo wafugaji watakuwa tayari kulima mazao ya malisho, itasaidia kuongeza wingi wa maziwa hapa nchini hivyo kuanzishwa viwanda vingi vya usindikaji maziwa pamoja na kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao.

Alisema kupitia mdahalo huo, wamepata fursa ya kujadiliana na kubaini changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo, ikiwamo ukosefu wa malisho.

“Tunaendelea kuhamasisha wafugaji nchini kuondokana na ufugaji wa mazoea kwa kutegemea malisho, huku mabadiliko ya tabia nchi yakichangia kupungua kwa malisho. Kupitia mdahalo huu, tutajitahidi kushirikiana,” alisema.

Mratibu Mwandamizi wa Shirika linalojihusisha na wadau mbalimbali kwenye sekta ya kilimo na ufugaji (Agri Pro Focus), Ernest Likoko, alisema wamekuwa wakishirikiana na wadau kuangalia changamoto zilizopo katika sekta hiyo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na kuikuza.

Alisema changamoto zilizoibuliwa katika mdahalo huo ikiwamo ukosefu wa malisho, zitapelekwa kwenye mkutano mkubwa wa wadau wa maziwa Afrika, Nairobi nchini Kenya baadaye mwezi huu.

Kuhusu hali ya unywaji maziwa nchini, Likoko alisema wanaendelea kuhamasisha wadau ili kusaidia maendeleo ya sekta hiyo sambamba na kuendeleza usindikaji wa maziwa kwenye viwanda mbalimbali.

Alisema lengo ni kuongeza idadi ya wanywaji maziwa kwani bado ni changamoto kubwa nchini.

“Tumejipanga kuanzisha jukwaa la wadau katika sekta ya maziwa, ambalo litaweza kuendeleza sekta hiyo sambamba na kuja na suluhisho la changamoto hizo.

“Jukwaa hilo litawajumuisha wafugaji, wakulima, wadau kutoka serikalini pamoja na mashirika binafsi,” alisema.

Meneja Msaidizi wa mradi wa kuongeza kipato na ajira kwa vijana na wanawake kutoka Shirika la Maendeleo la Uholanzi ( SNV), Paschal Tekwi, alisema bado kuna changamoto nyingi katika sekta ya mifugo.

Alisema kutokana na hilo, wamekuwa wakitoa mikopo kwa wanawake ili kununua vitendea kazi waweze kuendeleza sekta ya maziwa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles