26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wanaoharibu vyanzo vya maji waonywa

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Hamad Chande, amewaonya wanaofanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji waache mara moja ili kudhibiti athari za uharibifu wa mazingira kama mafuriko.

Chande amezungumza hayo mbele ya wakazi wa kijiji cha Misegese kilichopo wilayani Malinyi mkoani Morogoro ambacho kinakabiliwa na mafuriko kwa miaka mitano mfululizo kutoka kwenye mto Furua.

Mafuriko hayo yamesababishwa na shughuli za kilimo na ufugaji zinazofanywa ndani ya mita 60 kutoka kwenye mto huo.

“Kutunza mazingira iwe ni sehemu ya utamaduni wetu, kufanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji ni kuharibu mazingira na Serikali inapata hasara kugharamia miundo mbinu inayoharibiwa na mafuriko.

“Hivyo naviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuzuia wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye mto Furua ili kuzuia athari hizi zisiendelee kujitokeza,” amesema Chande.

Aidha Chande amewasihi wananchi wa kijiji cha Misegese kuwa wavumilivu wakati Serikali ikijiandaa kutatua tatizo hilo.

“Nawaagiza wataalamu kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuanzia sasa warudi kwa ajili ya kutathmini namna ya kurejesha mto kwenye asili yake hivyo nawaomba wananchi muwe wavumilivu”.

Chande ameongeza kuwa taka ni fursa ya ajira, wananchi wanapaswa kutumia kwa kuzibadili kuwa bidhaa kwani hiyo itasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira nchini.

” Natoa rai kwa wananchi kuchukulia taka kama njia ya kujiingizia kipato kwa kuzibadili kutoka taka mpaka kuwa bidhaa zingine, jambo hili litasaidia kutunza mazingira yetu yawe safi na salama,” amesema.

Nae Meneja NEMC wa Kanda ya Morogoro Rufiji, Amina Kibola, amesema maagizo aliyoyatoa Naibu Waziri watayafanyia kazi kwa kurudi kutathmini eneo lililoathirika na mafuriko na kuangalia namna ya kulikabili ili athari hizo zisiendelee kujitokeza.

Amina amesema ni lazima sasa wananchi wafuate miongozo, taratibu na sheria za matumizi bora ya ardhi ili kulinda mazingira yetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles