PASCHAL MALULU – KAHAMA
MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Anamringi Macha, ametangaza msako dhidi ya watu wanaolea watoto wasio wao kwa lengo la kuwafundisha kuwa ombaomba ili kujipatia kipato kisicho halali.
Hayo aliyasema jana mjini hapa, alipokuwa akipokea majina ya watu wanaoishi na watoto kwa lengo la kuwalea na kuwafundisha tabia ya kuombaomba mtaani ili kujipatia kipato.
Macha alisema Wilaya ya Kahama imekuwa na wimbi la watoto wengi wa mitaani.
Alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya imefuatilia na kubaini watoto hao wanachukuliwa kutoka wilaya za jirani na kuletwa Kahama kwa shughuli hiyo.
Macha alisema licha yakuwepo kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, lakini isiwe kigezo cha watu kujipatia kipato kisicho halali kwa kuwaajiri ili kuombaomba, hivyo watakaokamatwa sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Kuishi na mtoto ambaye si wako bila maelewano na wazazi pande zote mbili ni kosa kisheria, sambamba na kwamba umri alionao anatakiwa awe shule, hivyo Serikali ya awamu ya tano inahakikisha kila mwananchi anafanya kazi na kupata kipato kilicho halali,” alisema.
Alisema operesheni ya kuwasaka watu hao itaenda sambamba na kuwaondoa ombaomba wote waliopo Kahama Mjini na kuwapeleka katika maeneo maalumu ambayo yapo kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.