Majaliwa: Tunahitaji wawekezaji kilimo cha miwa

0
959

MWANDISHI WETU – DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Marcelino Medina Gonzalez na amewakaribisha Wacuba waje wawekeze kwenye sekta ya kilimo, hususan cha miwa.

Majaliwa alikutana na kiongozi huyo jana jijini Dodoma.

Aliishukuru Serikali ya Cuba kwa ushirikiano mzuri inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kuboresha maendeleo ya jamii.

“Tanzania na Cuba zina uhusiano wa kihistoria. Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, yaliyokuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Cuba, hayati Fidel Castro,” alisema.

Alisema Serikali ya Cuba imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa sukari, hivyo amewakaribisha Wacuba waje nchini washirikiane na Serikali ya Tanzania katika kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kuboresha kilimo cha miwa na kuanzisha viwanda vya sukari.

Majaliwa alisema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Serikali ya Cuba kwa kuwa ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano wa muda mrefu na Tanzania katika masuala ya kisiasa, kijamii, kiafya na kiuchumi.

“Mfano katika sekta ya afya, madaktari wengi kutoka Cuba wamekuwa wakija Tanzania kutibu wagonja waliokuwa na maradhi makubwa na pia Serikali ya Cuba imekuwa ikitoa fursa kwa Watanzania kwenda kusomea fani ya udaktari,” alisema.

Pia aliwakaribisha Wacuba waje wawekeze katika sekta ya utalii, hususani wa fukwe kwa sababu Tanzania ina fukwe nzuri.

Alisema mji mmoja wa Varadero wa nchini Cuba unaingiza watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu wa kilomita 22.

Akizungumzia kuhusu ofisi za ubalozi wa Tanzania zilizofunguliwa nchini Cuba, alisema zimesaidia kurahisisha mawasiliano kwa sababu awali kulikuwa na balozi mmoja tu ambaye alikuwa akiwakilisha nchi hiyo hapa nchini.

Naibu Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Gonzalez alisema Serikali ya Cuba itahakikisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unakuwa endelevu.

Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.

Alisema Serikali ya Cuba imefurahishwa na kitendo cha Serikali ya Tanzania kufungua ofisi ya ubalozi nchini Cuba kwa sababu imezidi kuimarisha mahusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.

Kiongozi huyo pia amefanya ziara Zanzibar kabla ya kuja Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here