Daktari bingwa aonya kutibu majeruhi wa moto kwa asali

0
935

AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM

DAKTARI bingwa wa upasuaji katika Hospitali  ya Taifa ya Muhimbili (MNH),  Endwin Mrema,  ameishauri jamii kuacha kumtibu majeruhi wa moto kwa asali na mafuta badala yake watumie njia ya kumwagia majeruhi maji zaidi ya dakika 15.

Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Saalam, alisema hatua hiyo inasaidia mwili wa mtu aliyeungua kupoa kutokana na joto alilopata.

“Kuna vitu watu wanafanya kutokana na kutokuwa na uelewa au elimu, mfano mtu akiungua wengine wanampaka  asali, kinyesi cha sungura, wengine unga wa muhogo, hivi vitu vyote havisaidii kwa mtu aliyeungua.

“Ukiona mtu kaungua moto mtoe mpeleke mbali na ummwagie maji kama dakika 15 hadi 20 kama amevaa saa, pete, cheni, hereni chochote kile cha chuma mvue kwa sababu mwili bado una joto na vitu vya chuma vinachukua muda mrefu kupoa, kumwagiwa maji itasaidia mwili kupoa haraka,” alisema Dk. Mrema.

Alisema baada ya majeruhi kupatiwa huduma hiyo awahishwe katika kituo cha afya kilichopo karibu ili aweze kupatiwa huduma za kitaalamu zaidi.

“Kwa matibabu ya kitaalamu huwa tunawapa maji, chumvichumvi, dawa za maumivu, kuna Cream ambazo tunawapaka, pia tunawafunga kwa gozi na bandeji. Upasuaji ni hatua ya baadaye kama itahitajika,” alisema.

Alishauri kuwa endapo mtu ataungua hata kwa kiwango kidogo asipuuzie, badala yake aende hospitali akapate matibabu  zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here