Sussan Uhinga na Oscar Assenga, Tanga
WIMBI la mauaji limeendelea kutikisha taifa baada ya usiku wa kuamkia jana watu wanane kuuawa kwa kuchinjwa, wakiwamo watatu wa familia moja katika Mtaa wa Mleni nje kidogo ya Jiji la Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,
Leonard Paul, alisema tukio hilo lilitokea saa 7 usiku katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, Manispaa ya Tanga.
Alisema watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walivamia makazi ya wananchi hao wakiwa wamelala usiku, kisha kuwateka na kuwapeleka hadi kwenye msitu na kuwaua kwa kuwachinja.
Kamanda Paul alisema watu hao wakiwa na mapanga na visu, walivamia nyumba tatu katika eneo hilo.
“Walianza kuvunja nyumba ya kwanza na kukuta watu watatu ambao waliwaua wote kwa kuwakata maeneo mbalimbali ya miili yao, kisha kuvamia nyumba ya pili na ya tatu na kufanya hivyo hivyo,” alisema.
Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, waliiba mchele, sukari na biskuti na kutokomea msituni karibu na maeneo ya Amboni.
Aliwataja waliouawa kuwa ni Mikidadi Hassan, Mussa Hassan na Mkola Hussein ambaye nyumba yake ilikuwa na duka dogo ambalo waliiba bidhaa zote.
Wengine ni Hamis Issa, Issa Ramadhani na wengine waliofahamika kwa jina moja ambao ni Kadri, Mahmoud raia wa Kenya na Salum ambaye ni mchunga ng’ombe.
Alisema hadi jana hakuna mtu aliyekamatwa, lakini Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali dhidi ya wahusika.
“Tunaendelea na msako mkali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuhakikisha watu hawa wanakamatwa,” alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Mzizima, Chiluba Frederick aliiambia MTANZANIA kuwapo na wimbi la watu ambao ni wahamiaji haramu wanaodaiwa kujificha kwenye mapango ya Amboni na kuendesha vitendo vya uhalifu.
Frederick alisema watu hao, walizingira nyumba tatu na kuwatoa ndani wananchi hao, kisha kuwapeleka msituni.
Alisema walishtushwa na mayowe ya wananchi kuomba msaada usiku, lakini walipofika eneo la tukio walikuta tayari wamepoteza uhai kwa kukatwa katwa kwa mapanga.
“Ni tukio la kusikitisha, waliwatoa kwenye nyumba na kuwapanga mstari, kisha kuanza kuwachinja kwa kutumia mapanga na visu kama kuku na kuwakata sehemu mbalimbali za miili yao, tulishindwa kuwasaidia, hatukuwa na silaha za aina yoyote ile,” alisema Frederick.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mleni, Shabani Muumini, alisema wananchi wengi wamekumbwa na hofu kubwa na kuviomba vyombo vya usalama kuchukua hatua haraka.
Alisema licha ya kuwapo askari wengi, wakiwamo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hali bado ni tete.
“Ndugu waandishi kama mnavyotuona, tumekaa makundi makundi tunahofia usalama wetu, wananchi wengi hawana amani, wameshindwa kufanya shughuli za maendeleo,” alisema Muumini.
Alisema wiki mbili zilizopita kata hiyo ilivamiwa na watu wasiofahamika, ambao waliiba kuku 40, ng’ombe na mbuzi jambo lililosababisha wananchi wengi kukimbia maeneo yao wakihofia usalama.
Mkazi mwingine, Pili Selemani alisema wana wakati mgumu kutokana na kushindwa kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.
“Hakuna biashara wala kulima, tunaogopa kwenda kuchota maji, ukiacha mauaji haya, hivi sasa kuna matukio mengi ya wanawake kubakwa na watu wasiofahamika,” alisema Pili.
Mke wa marehemu Mkola Hussein, Asha Saidi (20), alisema watu walifika ndani kwao saa saba usiku na kujitambulisha wao ni polisi.
Alisema watu hao waliokuwa wamevalia mavazi meusi walianza kumpiga mume wake, huku wakimtaka awaeleze mahali watoto wake walipo na asipofanya hivyo watamuua.
Karibu miezi mitatu sasa, eneo hilo limekuwa likilindwa na vyombo vya dola.
Mauaji haya ni mfululizo wa matukio ya kinyama ambayo yametokea wilayani Sengerema mkoani Mwanza, ambako watu saba wakiwamo watano wa familia moja waliuawa kwa kuchinjwa na wiki moja baadae watu wengine watatu walivamiwa na kuchinjwa ndani ya msikiti.