Na Clara Matimo, Mwanza
Zaidi ya wananchi 25,000 wa Kata ya Buzilasoga wilayani Sengerema mkoani Mwanza wanatarajia kunufaika na huduma za afya baada ya zahanata hiyo iliyopo Kijiji cha Kanyerere kuanza kutoa huduma za msingi ndani ya siku 14 zijazo.
Kituo hicho ambacho kimejengwa kwa gharama ya Sh milioni 481,881,697.70 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) kitaanza kutoa huduma kwa wananchi ndani ya wiki mbili baada ya agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa kutaka huduma zianze kutolewa kituoni hapo huku wakisubiri huduma zingine ziendelee kukamilika taratibu.
Akizungumza wilayani humo Desema 16, 2023 baada ya kutembelea kituo hicho na kukikakagua ambacho ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 96 Waziri Mchengerwa amesema wakina mama wajawazito wanaweza kuanza kupata huduma kituoni hapo wakati wanaendelea kukamilisha mapungufu madogomadogo yaliyopo.
“Ndani ya wiki mbili kuanzia leo nataka jengo hili lianze kutumika hawa wananchi wanapaswa kupata huduma za afya karibu, mganga mkuu wa wilaya hakikisha ndani ya wiki mbili ulete wataalamu wa afya ambao wataanza kutoa huduma kidogokidogo .
“Mwezi wa pili mwaka kesho serikali itaongeza ajira kwa ajili ya watumishi wa umma zaidi ya 25,000 katika sekta ya afya na elimu hivyo tutaongeza watumishi wengine hapa endapo itahitajika,” alisema Waziri Mchengerwa na kuongeza.
“Msiwanyime haki watanzania, ambao Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anapambana usiku na mchana kuhakikisha anawatatulia changamoto zinazowakabili katika sekta mbalimbali, mjiongeze, ukiwa kiongozi ni kuwa mbunifu, kujiongeza kuwa na kuwa na huruma dhidi ya wananchi wanaosafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, ujue mahitaji ya wananchi na lazima ujue kuwahudumia wananchi,” alisema.
Agizo hilo la Waziri Mchengerwa limekuja baada ya ombi la Mbunge wa Sengerema Hamis Mwagao(Tabasamu) aliyehoji kwa nini kituo hicho cha afya hakianzi kutoa huduma kwa wananchi wakati ujenzi wake umeishakamilika.
Hata hivyo, akimueleza Waziri Mchengerwa kwa nini kituo hicho hakijaanza kazi ingawa kimeishakamilika kwa asilimia 96, Mratibu wa TASAF Wilaya ya Sengerema Malissa Ndugha, alisema utaratibu wa fedha za mfuko huo unawataka wananchi wachangie asilimia 10 ya fedha za mradi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema, Binuru Shekidele, alisema Kata ya Buzilasoga ina vijiji vitano lakini wananchi wa vijiji vitatu ndiyo waliochangia na vijiji viwili hawakuchangia hivyo kusababisha kukwama kwa fedha za kukamilisha mapungufu yaliyopo kwenye mradi huo.
Wakizungumza na Mtanzania Digital baada ya Waziri Mchengerwa kutoa siku 14 kituo hicho kiwe kimeanza kutoa huduma, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kanyerere akiwemo, Metilda Mpina, Winfrida Kabipi na Regina Kayobe, walimpongeza kiongozi huyo na kubainisha kwamba itawaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kwenda Kijiji cha Igaka kufuata huduma za afya.