23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wazuia msafara wa Kinana

kinanaNA ELIYA MBONEA, BAHI
MAMIA ya wananchi katika Kata ya Msisi, Wilaya ya Bahi, Mkoa wa Dodoma, wamesimamisha msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, wakitaka kupata ufafanuzi wa majengo ya Shule ya Msingi Msisi yaliyoezuliwa na mvua mwaka 2011.
Kinana alikutana na hali hiyo juzi saa 12:30 jioni alipokuwa akitoka katika vijiji vya Kongogo, Chonde, Irindi, Nguju na Lamaiti akielekea mjini Dodoma.
Kinana yuko mkoani Dodoma kushiriki shughuli za maendeleo, kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM na kuzungumza na wananchi.
Baada ya kiongozi huyo kusimamishwa na wananchi hao, baadaye walielekea katika shule iliyoezuliwa wakiwa pia na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye.
Baada ya kufika shuleni hapo, mkazi wa Kijiji cha Msisi, Robert Zakayo, alisema kwa niaba ya wenzake kwamba wameamua kuzuia msafara huo ili kufikisha kilio chao cha muda mrefu kwa kuwa hakuna dalili za majengo yaliyobomoka kukarabatiwa.
“Pamoja na ujio wa wageni wa mkoa, wageni wa kitaifa na hata wageni wa shirika la msaada mwekundu, bado sisi wananchi wa Msisi tumeendelea kupoteza matumaini ya watoto wetu kupata elimu bora.
“Kwa maana hiyo, tunaomba utupatie majibu hiyo shule itajengwa lini ili watoto wetu wawe na matumaini ya kupata elimu bora,” alisema Zakayo.
Akijibu malalamiko hayo, Kinana alimhoji Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Hussein Kamau, ni kwanini majengo hayo hayajajengwa ingawa yameezuliwa muda mrefu.
Akitoa maelezo kwa Kinana, Kamau alisema majengo hayajaezekwa upya kwa sababu utaratibu unaandaliwa ili yajengwe upya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles