WASANII wa bendi ya Yamoto Band wameweka wazi kwamba hakuna msanii asiyependa kuwa na mafanikio kama ya Nasib Abdul (Diamond) anayezidi kung’ara katika muziki wake. Kauli hiyo waliitoa jana walipotembelea Kampuni ya New Habari (2006) Ltd iliyopo Sinza Kijiweni jijini Dar es Salaam, ambayo huchapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa, Dimba na The African. “Ukweli ni kwamba, hakuna asiyependa kuwa na mafanikio makubwa kama anayopata Diamond katika muziki na hali hiyo ndiyo inayotupa hamasa sisi Yamoto Band kujituma zaidi ili tufikie mafanikio yake,’’ alieleza Dogo Aslay. Kundi hilo linaloongozwa na Said Fella lenye maskani yake Temeke lilieleza kwamba, ili wasanii waweze kufanya kazi na wasanii wa nje kwa mafanikio lazima wajitangaze kwanza katika nchi zao. “Sisi leo tumeshirikiana na wasanii mbalimbali wa kimataifa akiwemo Yemi Alade, lakini kama haujulikani katika nchi yako na hujajitangaza kwa kufanya maonyesho mbalimbali nchi za nje hata ukishirikiana na msanii gani hautofanya vizuri, kinachotakiwa ni kujituma, kujitangaza, ndipo ushirikiane na wasanii wa kimataifa kama tunavyofanya sisi,’’ alifafanua zaidi Aslay.