25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi watishwa kunyang’anywa uraia

Na Elias Msuya, Katavi

MAKADA wa Umoja wa Katiba ya Wananchi, (Ukawa), wamewataka wananchi wa Jimbo la Nsimbo mkoani Katavi, kutotishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa  watanyang’anywa uraia endapo watamchagua mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Akizungumza na wananchi wa iliyokuwa kambi ya wakimbizi ya Katumba jana, Katibu wa Chadema Mkoa wa Katavi, Almas Ntije alisema CCM imekuwa ikiwatisha wananchi hao waliopewa uraia mwaka jana, kuwa watanyang’anywa uraia wao kama watachagua wagombea wa Ukawa.

Kabla ya kambi hiyo na ile ya Mishamo mkoani hapa, zilitaka kutolewa kwa wawekezaji wa kampuni ya Agrisol ya Marekani, lakini uwekezaji ukashindikana kutokana na malalamiko ya wananchi.

Ntije, alisema Serikali ya CCM ilitaka kuuza kambi hizo kwa masilahi binafsi, lakini vyama vya upinzani vilipinga.

“Kuna vitisho vingi vinatolewa kwenu ili msivipigie kura vyama vya upinzani. Wasiwatishe kwa sababu uraia huu ni haki yenu. Kuna nchi zaidi ya saba zimehusika na Umoja wa Mataifa ili mpewe uraia mlio nao,” alisema Ntije.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Issa Mohamed Said aliwataka wananchi wananchi wa jimbo hilo kuikataa CCM kwa sababu ni sawa na mti wenye mashetani unaowasumbua kwa muda mrefu.

“Leo ni mwaka wa 54 tangu uhuru wa Taifa hili, linatawaliwa na CCM. Kila wakija hapa wanasema watawajengeeni barabara, maji na umeme, lakini hawatekelezi.

“Ukimchagua Lowassa, kipaumbele cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na tatu ni elimu. Uwe Mtanzania wa kabila lolote utapata elimu kuanzia awali hadi chuo kikuu bure,” alisema Issa.

Alisema CCM imewafanya wananchi kuwa mtaji wa kutajirika kutokana na fedha zilizoletwa na Umoja wa Mataifa  kwa ajili ya kuwahudumia waliokuwa wakimbizi huku wakiwaacha wakiwa na umasikini wa kutisha.

“Wao wanajenga maghorofa Dar es Salaam, ninyi mnaendelea kuwa masikini hapa. Hii barabara ilishatangazwa kuwa itajengwa kwa lami, hadi leo haijajengwa. Tukiingia madarakani kesho yake tunatangaza elimu bure shule zote,” alisema Issa.

Huku akitoa mfano wa Rais Jakaya Kikwete, Issa alisema Serikali ina fedha nyingi za kuwezesha elimu na afya kutolewa bure.

“Rais Kikwete anapokea mshahara mnono kila mwezi na kila akisafiri nje ya nchi analipwa posho kubwa na ndiye rais aliyetumia muda mwingi nje ya nchi.

“Halafu tukisema tutatoa elimu bure, wanauliza fedha tutatoa wapi, wakati fedha wanazitumia ovyo. Fedha nyingine zimepotelea kwenye ufisadi wa akaunti ya Escrow, mawaziri wamejiuzulu ndiyo adhabu yao,” alisema.

Naye Katibu Uenezi wa Braza la Vijana la Chadema (BAVICHA), Edward Simbei alisema amesikitishwa na vitisho vya makada wa CCM kwa wananchi wa jimbo hilo.

Aliwataka wananchi  kumkataa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli ambaye alikuja mkoani humo kutoa ahadi zilizowahi kutolewa na marais waliopita, lakini hazitekelezeki.

“Magufuli hawezi kuleta mabadiliko, CCM ni ile ile, ndiyo maana mnaona Lowassa na Sumaye wamejitoa ili kuleta mabadiliko,” alisema Simbei.

Naye mbunge wa zamani wa Jimbo la Mkanyageni Zanzibar, Habib Mnyaa aliwataka wananchi hao kujisikia kama Watanzania wengine kwa sababu ni haki yao.

Alisema CCM wanawatisha ili wakae madarakani kwa muda mrefu. “Tanzania imetoa ardhi na huduma ndogo ndogo, UNHCR ndiyo inawahudumia, hata hao askari wanalipwa na hao. Hamkupaswa kuishi kwenye nyumba kama hizi,” alisema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Gerald Kitabu alisema anatambua kero za wananchi hao kuwa ni pamoja na barabara na migogoro ya ardhi na kwamba atazitatua akichaguliwa.

“Natambua kero za wananchi wa Jimbo la Nsimbo, kwanza kuna kero ya barabara, mkiinichagua na madiwani wangu tutamaliza kero hiyo. Najua wengi mnazunguka ili kufika mjini mimi nitaweka daraja ili njia iwe fupi,’ alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles