29.9 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yaiteka ngome ya CUF

Pg 3Waandishi Wetu, Zanzibar na Dar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimeitikisa ngome kuu ya Chama Cha Wananchi (CUF) kwenye mkutano wa ufunguzi wa kampeni uliofanyika Kisiwa cha Pemba.

Pemba ni ngome ya chama hicho cha upinzani visiwani Zanzibar kutokana na kuwa na nguvu kubwa,  huku CCM ikiwa na mizizi Unguja.

Mkutano wa CCM uliofanyika jana katika Uwanja wa Gombani ya Kale Mkoa wa Kaskazini Pemba Wilaya ya Chakechake, inaweza kutafsiriwa kuwa ilitingishwa kutokana na umati mkubwa uliojitokeza uwanjani hapo ukiwa na hamasa.

Dalili za mafanikio ya mkutano huo zilianza saa sita mchana ambako wananchi wengi walianza kuingia uwanjani hapo kutoka sehemu mbalimbali.

Vijana, wazee na akina mama walionekana wamevalia mavazi ya kijani na njano yenye nembo za CCM huku wakiimba na kushangilia wengine wakizunguka uwanja mzima kabla na baada ya kuwasili kwa mgombea urais wa chama hicho, Dk. Ally Mohamed Shein.

Mkutano huo unatajwa kuwa ni mkubwa kuwahi kutokea katika kampeni za miaka ya karibuni, ambapo CCM haikuwa na uungwaji mkono kama ilivyo sasa.

Baadhi ya wananchi walilieleza MTANZANIA kuwa mafanikio hayo ya kisiasa kwa CCM yametokana na uongozi mzuri wa Rais wa Zanzibar, Dk. Ally Mohammed Shein ambaye katika kipindi chake cha miaka mitano ameweza kuondoa uhasama uliokuwapo baina ya CCM na CUF.

Mzee Othuman Salehe Khamis (65) alisema katika kipindi cha miaka mitano ya Dk. Shein Kisiwa cha Pemba kimekumbukwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kujenga miundombinu ya barabara, umeme na maji katika maeneo ya vijijini.

“Hivi sasa Pemba imetulia, watu wanaishi kwa kuaminiana, miundombinu imejengwa, hospitali tukienda kuna dawa za wazee tofauti na miaka iliyopita ambapo uhasama wa kisiasa ulikuwa mkubwa na kuwafanya wananchi kutokuzikana na kushirikiana kwenye misiba,” alisema.

Baadhi ya vijana waliojitambulisha kuwa ni wanafunzi wa sekondari, walisema watafurahi kama Serikali ijayo itaweza kujenga vyuo vya ufundi stadi katika kisiwa cha Pemba ili waweze kupata ujuzi wa masuala mbalimbali ikiwamo ujasiriamali pindi wanapomaliza elimu ya msingi na sekondari.

Shein aahidi neema

Mgombea urais Zanzibar kwa CCM, Dk. Ally Mohamed Shein, alisema endapo atashinda wafanyakazi wataongezewa mshahara kutoka Sh 300,000 ambayo ndiyo kima cha chini kwa sasa hadi Sh 500,000.

Alisema ameweza kutekeleza mambo mengi aliyoahidi katika ilani iliyopita ya mwaka 2010/15 kwa kiasi cha asilimia 90 na kwamba asilimia 10 iliyobaki hajashindwa kuimalizia na kwamba tayari ameanza kuyatekeleza.

“Nilisema nitatekeleza kwa vitendo muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa, nawaahidi kuwa nitafanya makubwa iwapo nitashinda, wafanyakazi niliwaahidi kuongeza mishahara na katika kipindi cha miaka mitano nilifanya marekebisho kadhaa kwa awamu tatu  ambazo ni 2011/13 na 2014/15.

“Katika kipindi hicho nilibadili na kutengeneza upya miundo ya utumishi na tumeweka utaratibu mzuri ili kila mtu ajue haki yake, vyama vyenu vilitaka niongeze katika kipindi kile nikawaeleza kuwa wanivumilie.

“Sasa natamka wazi leo (jana) kwamba nitaongeza kutoka 300,000 hadi 500,000… inawezekana kwani uchumi wetu unakuwa vizuri na kila mmoja wenu afanye kazi kwa bidii na uadilifu ili nchi yetu isonge mbele,” alisema.

Alisema pia atahakikisha kuwa anasimamia ujenzi wa bandari pamoja na uwanja wa ndege wa Karume ili kuinua uchumi wa nchi hiyo.

Alisema mipango ya ujenzi wa bandari mpya na ya kisasa imekamilika kwani tayari serikali ya China imeshatoa msaada wa mkopo nafuu na watashirikiana na kampuni ya moja ya ujenzi nchini humo kukamilisha ujenzi wake.

“Tutaweka miundombinu ya kisasa na katika eneo la uwekezaji la Micheweni na tutajenga mji mpya wa kisasa wenye viwanda pamoja na nyumba ambazo zitauzwa kwa raia, tutaingia ubia na kampuni ya Azam ili tujenge uwanja mkubwa wa kisasa na wa aina yake wa kuchezea mpira,” alisema.

Alisema serikali itaendelea kusaidia wakulima ili waendelee kupata mafanikio kutokana na mazao yao.

“Serikali iliahidi kuwapatia ruzuku wakulima wa mpunga, tuliwasaidia kupata mbegu bora, mbolea pamoja na dawa za kuulia wadudu kwa kuchangia  kiasi cha asilimia 75 huku wakulima wakichangia asilimia 25,” alisema.

Alisema mpango huo wa kutoa ruzuku umewawezesha wakulima kuvuna kiasi cha tani 33,000 kutoka 21,000, mwaka 2012, katika zao la karafuu walikuwa wakiuza kwa Sh 5,000 lakini mauzo yamepanda hadi kufikia 14,000.

“Karafuu inayouzwa nje ya nchi imefikia kiasi cha tani 5.340 jambo ambalo halijawahi kutokea na tulitwanga hadi maganda yake tunakunganisha, tutaendelea kufanya utafiti kujua mbegu bora ili tuweze kuinua kilimo chetu,” alisema.

Alisema ili kuendeleza mapambano dhidi ya umaskini serikali yake itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo mpango wa awamu ya tatu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf)…..

Alisema iwapo atachaguliwa atahakikisha Zanzibar inafikia katika uchumi wa kati kwa kuinua pato la kila mwananchi Sh bilioni 1.3 na hadi kufikia kiasi cha Sh. bilioni 1.560 na kwamba itakapofika mwaka 2020 atahakikisha inafikia Sh bilioni 3.

“Vijana msidanganyike wale wanaokuja na kuwaeleza kuwa watawapatia ajira ni waongo, si rahisi kutengeneza ajira kwa mwaka hata miaka mitano, mimi tayari nimeanzisha mfuko wa kuwawezesha ili mpate mikopo na mjiajiri wenyewe lakini pia tutajenga viwanda, msikubali kupewa ahadi hewa,” alisema.

Balozi Karume

Awali akizungumza katika mkutano huo, Balozi Ally Karume alimtupia kijembe mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) chini ya mwamvuli wa Ukawa, Maalim Seif Sharif Hamad akisema kuwa  hawezi kuongoza nchi hiyo.

Balozi Karume alisema Maalim hawezi kuongoza kutokana na kwamba si mvumilivu, mstahimilivu na wala hapendi ushirikiano na viongozi wenzake.

“Mimi ni msomi naelewa, yule bwana anayetaka kuwa rais wa nchi hii hawezi kuongoza kwani si mvumilivu, mstahimilivu na hapendi ushirikiano.

“Dk. Ally Mohamed Shein namjua vizuri anaweza kutuongoza vyema 2015 hadi 20… nimempima ana uwezo na uzoefu, tusitafute mtu mwingine anayetaka kufanya majaribio hilo haliwezekani,” alisema.

Maua Daftari

Akizungumza katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, Dk. Maua Daftari aliwataka Wazanzibari kumchagua Dk. Shein kwani ni mwadilifu, mkweli na mchapakazi.

“Mchagueni Dk. Shein si mwongo akisema anafanya kitu, anafanya kweli tulikuwa hatuna huduma ya maji akaleta, barabara zilikuwa mbovu akasimamia zikajengwa na hata vituo vya afya vimejengwa,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Veronica Romwald, Asifiwe George, Dar es Salaam na Arodia Peter, Pemba

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles