26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi watakiwa kushiriki mapambano ya Rushwa

Na Samwel Mwanga, Maswa

Wananchi wameaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia na siyo kuiachia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) katika mapambano hayo.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Takukuru wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Petro Horombe wakati wa maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za binadamu yaliyofanyika katika viwanja vya Stendi ya zamani mjini Maswa.

Amesema njia sahihi ya kuleta maendeleo nchini ni ushiriki wa kila mwananchi kuwafichua wala rushwa na kutoshiriki vitendo vya rushwa na kuwataka kutoa taarifa za vitendo vya rushwa katika ofisi za Takukuru kwa njia ya kupiga simu au kufika ofisini.

Aidha, ametumia muda huo kuwaomba watumishi wa Umma kufanya kazi zao za kuwahudumia wananchi kwa uadilifu  kwa kufuata viapo vyao vya kazi na wale ambao watakiuka na kujihusisha na vitendo vya rushwa Takukuru itawashughulikia kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine Horombe amewapongeza walimu walezi na wanafunzi wa shule za msingi Binza, St. Bakhita na Nyalikungu zilizoko mjini Maswa zenye Klabu za wapinga rushwa walioshiriki katika maadhimisho hayo na kutoa ujumbe mbalimbali juu ya mapambano ya rushwa katika jamii kwa njia ya mabango, nyimbo na ngonjera.

Wanafunzi hao wapatao 58 kila mmoja alipatiwa daftari moja na kalamu ikiwa ni sehemu  ya Takukuru wilaya ya Maswa kutambua mchango wa wanafunzi hao juu ya mapambano ya rushwa.

Awali wanafunzi hao pamoja na watumishi wa Taasisi hiyo waliandamana kutoka ofisi za Takukuru wilayani humo hadi kwenye viwanja vya Stendi ya Zamani mjini Maswa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles