Na Sheila Katikula, Mwanza
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Fabian Masaga, amewataka wananchi kuweka utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuepuka kuishi na mrundikano wa magonjwa mwilini.
Masaga amesema hayo jana katika sherehe za maadhimisho ya kutimiza miaka 50 ya hospitali hiyo yanayolenga kuendeleza huduma bora kwa wananchi kwenye Uwanja wa Furahisha mkoani hapa.
Amesema afya ni kitu muhimu na ndiyo chanzo cha kukuza uchumi wa taifa hivyo wananchi wawe na utaratibu wa kupima afya zao ili waweze kubaini magonjwa yanayowakabili.
Naye Profesa William Mahalu Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa moyo na vifua amesema wananchi wachangamkie fursa hiyo ambayo itawawezesha kupima maradhi mbalimbali bila gharama yoyote.
Amesema wameamua kusherehekea kutimiza miaka 50 ya hospitali hiyo kwa njia ya kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwapima magonjwa ya macho, meno,kisukari, na figo kuanzia Novemba 3 -5,2021.
Amesema wamepita katika mikoa ya Geita, Shinyanga,Mara na Simiyu na kuwahudumia jumla ya wagonjwa 1896 na kufanya upasuaji kwa watu 240 huku wengine wakiwapa rufaa ya kwenda hospitali ya Bugando.
Amesema hospitali hiyo inajivunia kuwa na kipimo cha juu zaidi cha MRI wamekipata hivi karibuni ambacho kina wasaidia wagonjwa kupata vipimo mbalimbali vya magonjwa ya ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa huduma za tiba wa hospitali ya rufaa ya kanda ya Bugando Dk. Bahati Wajanga, amesema kupima magonjwa kabla ya kuugua husaidia kuchukua hatua sitahiki ikiwa ni pamoja na kupata ushauri na matibabu.