27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WANANCHI WASHAURIWA KUSOMESHA WATOTO WAO

Na ASHURA KAZINJA-MOROGORO

WANANCHI mkoani Morogoro wameshauriwa  kujiendeleza kielimu na wakumbuke kuwapeleka watoto wao shule ili wapate elimu itakayowawezesha kukabiliana na changamoto za maisha.

Hayo yalielezwa jana na Diwani wa Kata ya Mkambarani, Mohamed Mzee (CCM), wakati akizungumza na MTANZANIA mjini hapa.

Alisema kwamba, jamii inatakiwa kubadilika kwa kuipenda elimu kwa kuwa bila elimu, hakuna maendeleo yanayoweza kufanyika.

“Zama hizi siyo sawa na zama za zamani ambapo elimu haikutiliwa mkazo, hasa mkoani hapa. Siku hizi mambo yamebadilika, kwani bila elimu ni vigumu kuwa na maisha bora au kumudu upinzani wa ajira na biashara.

“Nayasema haya kwa sababu wananchi wengi mkoani hapa Morogoro, hasa hasa vijijini, hawana elimu ya kuwawezesha kumudu maisha yao ipasavyo.

“Pamoja na kutokuwa na elimu, bado wengi wao wamekuwa hawaoni umuhimu wa kuwapa elimu watoto wao, ingawa siku hizi kuna shule za kata na kuna sheria inayolazimisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule, waende shule kusoma,” alisema Mzee.

Pamoja na hayo, alisema kitendo cha Wilaya ya Morogoro Vijijini kutokuwa na shule za Serikali kwa ajili ya kidato cha tano na sita, kinasababisha wanafunzi wengi kuishia kidato cha nne.

“Wanafunzi wengi wanaishia kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita kwa kuwa wazazi wanashindwa kumudu gharama za kuwasomesha katika shule za mbali au kulipa ada kwenye shule binafsi.

“Hata hivyo, nashukuru kwa jitihada zinazofanyika za kuifanya Shule ya Sekondari Nelson Mandela iliyoko katika Kijiji cha Mkambarani, kuwa na kidato cha tano na sita,” alisema Mzee.

Wakati huo huo, diwani huyo aliwapongeza baadhi ya vijana katani kwake kwa kile alichosema wamekuwa na mwamko wa kufanya kazi, tofauti na zamani ambapo walikuwa wakinywa pombe za viroba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles