Na ERICK MUGISHA (DSJ) – DAR ES SALAAM
WANANCHI wa Mtaa wa Makangarawe Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam wamepinga kuhamishwa makaburi wanayotumia kuzikia kupisha ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Wakizungumza na MTANZANIA jana baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema eneo hilo awali lilikuwa linamikiwa na mtu binafsi aliyeamua kulitoa kwa wananchi litumike kuzikia.
Kwa mujibu wa wananchi hao, hadi sasa eneo hilo lina zaidi ya makaburi 300 hivyo wanapinga uamuzi huo wa kutaka kuyahamiasha.
Mkazi wa eneo hilo, Mohamedi Matope, alisema yeye na wenzake watano walikwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,m kufikisha kilio chao lakini walijikuta wakigonga mwamba baada ya kuambiwa kiongozi huyo yupo kwenye vikao na kutakiwa kurejea baada ya wiki mbili.
Naye Abdalah Katuni alidai kuwa mwenyekiti wa mtaa amekuwa akiwaendesha kwa mabavu ambako wao wanaopinga wamekuwa wakipokea vitisho kutokana na msimamo wao wa kuhamishwa makaburi hayo.
MTANZANIA ilifika katika ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Makangarawe na kuzungumza na na mwenyekiti wa mtaa huo, Denis Moyo.
Alisema suala la kuhamishwa makaburi hayo linatokana na uamuzi wa Manispaa ya Temeke ambayo imedhamiria kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa uwanja wa mpira, soko a na hospitali ya kisasa katika eneo hilo.
“Ninachofahamu hapa kuna mradi mkubwa na Benki ya Dunia ambayo ipo tayari kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake. Jambo lolote linapokuja ni lazima watakuwapo wanaopinga na wanaohitaji kuwapo kwa maendeleo ya eneo letu.
“…hiki ndicho ninachofamu ila kama unataka maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ambaye ofisi yake inasimamia suala hili,” alisema Moyo.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kupata ufafanuzi kuhusu suala hilo hakupatikana na MTANZANIA inaendelea na juhudi za kumtafuta kupata ufafanuzi wa kina wa suala hilo ikiwamo kuhamishwa makaburi hayo.