Na Mwandisho Wetu, Dodoma
Wananchi mbalimbali wa Jiji la Dodoma wamejitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) ambapo mgeni rasmi alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai.
Maadhimisho hayo ya Wiki moja yaliyobeba Kaulimbiu ya ‘AZAKI NA MAENDELEO’ yalianza kwa matembezi maalum yaliyoanzia katika Shule ya Sekondari ya Dodoma na kuelekea katika viwanja vya ukumbi wa Jakaya Kikwete ambapo ndipo kulipofanyika shughuli za ufunguzi.
Aidha, katika matembezi hayo yaliyofana sana washiriki walibeba mabango mbalimbali yenye jumbe tofauti za shuguli zinazofanywa na Mashirika ya Asasi za Kiraia ambazo zimekuwa na mchango mkubwa kwa Jamii ya watanzania na Taifa kwa ujumla.
Baadhi ya washiriki wa Matembezi hayo wamesema kuwa wameshiriki kwenye wiki ya Azaki mwaka huu kwaajili ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kufahamu shughuli zao ambazo kimsingi zimejikita katika kuwasaidia kupaza sauti zao na kuibua changamoto katika jamii ili Serikali iweze kuzifanyiakazi, na kwamba wao kama Azaki wanaona kuwa ushiriki wao kwenye Wiki ya Azaki utawapa fursa ya kuendelea kukuza mashirikiano baina yao.
Wiki ya AZAKI ni jukwaa pekee nchini linaloleta kwa Pamoja wadau wakuu wa maendeleo ikiwemo Serikali, Sekta binafsi na Asasi za Kiraia Pamoja na wananchi kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu ustawi wa nchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla ambayo imezinduliwa rasmi leo Jumamosi Oktoba 23, na kufungwa Oktoba 28, 2021.