29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wafunga mgodi wa Tanzanite

tanzanite

Na ELIYA MBONEA, Mererani

SHUGHULI za uzalishaji na uchimbaji wa madini ya Tanzanite katika mgodi wa Kampuni ya Sky Associate, zamani Tanzanite One katika mji wa Naisinyai Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, zimesimama kwa siku nzima jana baada ya wananchi kufunga mageti ya ofisi za mgodi huo.

Wananchi hao waliowasili kwenye mgodi huo  saa 10 alfajiri jana, walisababisha wafanyakazi waliokuwa wakibadilishana zamu kushindwa kuingia kazini kutokana na mageti kufungwa.

Hatua hiyo ya kufungwa milango na wananchi kushinda getini, ililazimu Jeshi la Polisi kufyatua mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya, lakini hatua hiyo haikufanikiwa kuwaondoa kwenye eneo hilo.

Hata hivyo, wakati askari wakifyatua mabomu, baadhi ya wananchi hususani wa kabila la Wamasai, walikuwa wakiwaeleza polisi kuelekeza mabomu hayo upande wao na si kufyatua kuelekea hewani.

Kuwapo kwa mgogoro huo kulisababisha uongozi wa Mkoa wa Manyara kufika kwenye eneo hilo wakiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Eliakimu Maswi, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Fransis Massawe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika eneo hilo, baadhi ya wananchi walidai kuwa tangu Kampuni ya Sky Associate ichukue uendeshaji wa mgodi huo, hakuna makubaliano ya shughuli za kijamii yaliyotekelezwa.

Wananchi hao waliyataja baadhi ya madai yao kuwa ni suala la ajira kwa wakazi wa kijiji hicho, uchangiaji wa huduma za kijamii kwa kijiji, tatizo la maji pamoja na suala la kupatiwa viroba vinane vya mchanga wa kuchambua kwa ajili ya wananchi wa Kijiji cha Naisinyai.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai, Taiko Laizer, alisema uongozi mpya wa kampuni hiyo haujatekeleza ahadi zake na wameshindwa kukutana na Serikali ya kijiji kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Akitoa ufafanuzi wa madai hayo mbele ya Maswi, wakurugeni wa kampuni hiyo walikiri kuwapo kwa tatizo lililochangiwa na ufinyu wa mawasiliano.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye kikao hicho, wakurugenzi wa Sky Associate, Faisal Shabhai na Hussein Gonga, walikiri kuwapo upungufu katika utekelezaji wa ahadi kadhaa kutokana na hali ya fedha katika kampuni hiyo.

Gonga alisema walikuwa wakikabiliwa na madeni waliyorithi zaidi ya Sh bilioni 12 na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mfuko wa Pensheni wa NSSF na wamelipa kiasi kikubwa cha madeni hayo. Baadaye waliahidi kutekeleza maazimio yote yaliyofikiwa katika kikao hicho.

Aidha walikubali ndani ya wiki moja kutoa kiasi cha Sh milioni 40 kama ahadi ya ujenzi wa madarasa, kuajiri watu 20 wa Kijiji cha Naisinyai.

Akizungumza katika kikao hicho, Maswi aliwataka viongozi wa Tanzanite One, kuimarisha uhusiano mwema na vijiji vinavyowazunguka pamoja na kuheshimu mikataba na Serikali za vijiji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles