23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WANANCHI WAFICHUE UOVU UNAOFANYIKA NDANI YA JAMII

NA CHRISTINA GALUHANGA                                

-DAR ES SALAAM

HIVI karibuni Jukwaa la Utu wa Mtoto lilifanya utafiti na kubaini kuwa Kata ya Kitunda iliyopo Wilaya ya Ilala inaongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwamo ukeketaji.

Hali hiyo imekuwa ikichangia ongezeko la ndoa na mimba za utotoni, wanawake kukosa elimu pamoja na ongezeko la magonjwa ya kuambukiza.

Mbali ya Serikali na taasisi binafsi kujitahidi kutoa elimu kuhusu athari za ukeketaji na mimba za utotoni, bado kuna makabila na mikoa inaendekeza utamaduni huo ambao umepitwa na wakati.

Inasikitisha kuona mkoa ambao wananchi wake wanaweza kufikiwa na taarifa nyingi kwa urahisi bado unaendeleza vitendo hivyo na wilaya zake zinakuwa kinara.

Utafiti huo umedhihirisha jinsi jamii inavyoendekeza vitendo vilivyopitwa na wakati hivyo, ipo haja ya serikali sasa kutunga sheria ambazo zitamkomboa mwanamke.

Kama hali iko hivyo kwa jiji la Dar es Salaam huenda tafiti za mikoa mingine zinaweza zikawa za kutisha na zenye athari zaidi kwa sababu wengi bado hawajafikiwa na elimu ya kujitambua na kutetea haki zao.

Hata hivyo jamii nayo imekuwa chanzo cha kuendelea kukithiri kwa vitendo hivyo kwa sababu ya kuficha maovu yanayoendelea kufanyika katika maeneo husika.

Jamii ingekuwa inatoa ushirikiano na kuacha kufumbia macho maovu au mila na desturi zilizopitwa na wakati katika maeneo yao vita ya kupinga vitendo hivyo ingekuwa na mafanikio.

Ninasema hivyo kwakuwa wapiga debe wengi wa vitendo hivyo hawaishi kwenye maeneo husika hivyo ushirikiano zaidi unahitajika kwa wananchi walio karibu kuibua na kufichua uovu unaofanyika ndani ya jamii inayowazunguka.

Ifike wakati kila mwananchi aone ana wajibu wa kupinga vitendo hivi ambavyo vimekuwa vikidhalilisha utu wa mwanamke na kumnyima haki zake za msingi.

Endapo kampeni ya kupinga vitendo hivyo itaendelea kufanywa na kundi dogo la watu, kamwe mila na desturi hizo haziwezi kuisha katika jamii zetu.

Ni imani yangu kuwa kampeni ili iwe endelevu na yenye matunda, mbinu mbadala na za kisasa zinahitajika kwa kujenga mtandao kuanzia ngazi za vijiji ili kila mmoja awe mpingaji mkuu wa vitendo hivyo.

Pia ni wakati sasa wa mashirika, asasi za kiraia na serikali kushirikiana na jamii hasa iishiyo vijijini kuwawezesha kupiga vita vitendo vya kikatili.

Imekuwa mazoea kwa baadhi ya asasi kuchukulia fedha za wafadhili na kuacha mzigo mkubwa kwa wanakijiji ambao wamekuwa wakikosa hata Sh 500 ya kupiga simu pindi panapotokea vitendo vya ukatili hali inayosababisha kampeni mbalimbali kukwama kwenye baadhi ya maeneo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles