Nyemo Malecela-Bukoba
WANAKIJIJI wenye hasira katika Kijiji cha Kishanda B, Kata ya Kibale, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, wanadaiwa kuvamia shamba la mwanakijiji mwenzao, Tryphone Jeremiah, kuchoma moto nyumba yake, kukata migomba na kuua mifugo yake wakiwamo mbuzi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Jeremiah alisema tukio hilo limefanyika Jumapili iliyopita wakati akiwa katika ibada kanisani.
Alidai kuwa wananchi hao takribani 200, walivamia mashamba na mifugo hiyo saa sita mchana baada ya kuwepo mgogoro wa ardhi baina ya baba yake na wanakijiji hao tangu mwaka 2007.
“Wananchi wanalalamika kuwa ninamiliki ardhi kubwa, baada ya wanakijiji hao kuvamia mashamba kwa makundi makundi, waliyafyeka kwa muda fupi na kuua mbuzi na kuwachoma moto pamoja na kubomoa nyumba,” alidai.
Mtoto wake, Ezla Tryphone, alidai kuwa wakati wanakijiji hao wanatekeleza unyama huo, wachungaji wa mifugo pamoja na mdogo wake Erneus Tryphone walikimbia na kujificha kwa sababu wananchi hao walikuwa wakisema yeyote atakayejitokeza watamuua.
Ezla alidai kuwa mashamba yaliyofekwa yalikuwa na ukubwa wa hekta 10.5.
“Mashamba hayo yalikuwa ni mali ya watu watatu, baba alikuwa na migomba na kahawa hekta tatu, mimi (Ezla) nilikuwa na hekta 1.5 na mdogo wangu (Erneus) hekta moja wakati shamba la miti yenye umri wa miaka sita lilikuwa na ukubwa wa hekta sita, mbuzi wengine walikamatwa na kuchinjwa na walichukua nyama,” alidai Ezla.
Mchungaji wa mbuzi hao, Fatius Mwesiga, alisema baada ya wanakijiji hao kuvamia, walijificha kuhofia usalama wao.
“Wananchi hao waliovamia walikuwa 200, walitumia saa tatu kutekeleza unyama huo, tulikuwa tumejificha kwani walikuwa wakisema tukijitokeza watatuua,” alidai.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kishanda B, Medius Atanas aliliambia MTANZANIA kuwa mgogoro huo ulitokana na mlalamikaji kujimilikisha ardhi kubwa, pia mifugo yake ilikuwa kero kwa wanakijiji.
“Mlalamikaji alikuwa na mgogoro wa muda mrefu na wananchi baada ya kujimilikisha eneo kubwa ambalo jingine halikuwa la kwake na yeye alikuwa akiishi Kitongoji cha Bugomora wakati mifugo yake ikiishi kitongoji kingine jirani,” alisema.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Ahmed Msengi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema mashamba yaliyoharibiwa ni migomba, kahawa na miti aina ya mipeini pamoja na kuwaua mbuzi wanne na kuwajeruhi mbuzi wawili.
“Kwa mujibu wa mlalamikaji (Jeremiah), anasema alikuwa na mbuzi 100, hivyo kati ya wale waliochinjwa na waliobaki hai wanaonekana 39 na mbuzi 57 hawaonekani kabisa,” alisema.
Msengi alisema chanzo cha mgogoro huo ni mlalamikaji kumiliki ardhi kubwa, mgogoro ambao tayari ulishafika mahakamani.
Alisema hadi sasa hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa baada ya watuhumiwa kukimbia, ingawa bado wanaendelea na msako kwa waliohusika na tukio hilo.