24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu: Maonyesho SADC fursa kwa Watanzania

Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema wiki ya maonyesho ya nne ya viwanda ya nchi za SADC ni fursa pekee ya kutangaza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mabanda kwenye maonyesho hayo yanayoendelea Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Maonyesho hayo ambayo yalifunguliwa juzi na Rais Dk. John Magufuli, yanafanyika katika maeneo matatu ambayo ni ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, viwanja wa Gymkhana na Karimjee.

“Nimekuja kufanya ufuatiliaji wa maandalizi ya mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi za SADC, nimekuta yanaendelea vizuri. Nimekuja kuangalia mwitikio wa wajasiriamali wa pande zote mbili za Muungano pamoja na wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa SADC, na pia mwitikio wa wananchi wetu ukoje,” alisema.

Waziri Mkuu alisema fursa hiyo ni muhimu kwa Watanzania kuonyesha bidhaa za ndani ili wageni wanaokuja wajue kuna bidhaa zipi zinazalishwa nchini.

“Tumetoa fursa kwa nchi za SADC zote, nao pia waonyeshe bidhaa zao. Maonyesho haya ni ya wazi, Watanzania wanayo nafasi ya kuja kuona na kujifunza,” alisema.

Alisema mbali ya fursa ya masoko, Tanzania inayo pia fursa ya kupata teknolojia mpya na za kisasa, ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa viwanda vya usindikaji bidhaa mbalimbali. “Tumeona utaalamu unaotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali, hii maana yake ni kwamba tunajifunza na teknolojia zinazotumika.

“Tunayo fursa ya kukaribisha viwanda kutoka nje ya nchi, wote hapa wameleta bidhaa zao.

“Pia tunawakaribisha waje waanzishe viwanda kwa ubia na Watanzania.

“Sisi tunayo ardhi, tunazalisha mazao mengi tu, kwa hiyo mbia wa nje anaweza kuunganisha mtaji na Mtanzania na wakajenga kiwanda hapa nchini,” alisema.

Mbali ya fursa za kiuchumi kwao binafsi, Waziri Mkuu aliwataka washiriki wa maonyesho hayo, watangaze vivutio vya utalii vilivyopo nchini, ambavyo vitasaidia kuwafanya wageni wanaoshiriki mkutano huo watamani kubaki nchini na kuvitembelea.

“Watanzania tutumie nafasi hii kutangaza vivutio vingine tulivyonavyo. Mbuga za wanyama tunazo nyingi, tunao Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika na huwezi kuupanda kutokea popote. Ili uupande, ni lazima uje Tanzania.

“Pia tuna eneo maarufu la Olduvai Gorge ambalo ni chimbuko la binadamu wa kwanza duniani, na hili liko Ngorongoro. Tuna fukwe nzuri, zenye mchanga mzuri ambazo ukikaa wala huwezi kuchafuka, zina urefu wa zaidi ya km. 1,400 kutokea Tanga hadi Mtwara,” alisema.

Mapema, Waziri Mkuu alifanya kikao na mawaziri wa mambo ya nje, utumishi na utawala bora, viwanda na biashara wa Tanzamia, viwanda, biashara, wazee wa Zanzibar, naibu mawaziri wa Tamisemi, mambo ya nje na mifugo na uvuvi na kuwapa maelekezo ya kuboresha maandalizi hayo.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na makatibu wakuu wa wizara hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles