29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi vijiji 32 watamani kumwona JPM

ELIUD NGONDO, MBARALI

 WANANCHI wa vijiji 32 vya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya vilivyokuwa vinatakiwa kuondolewa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wamesema wanatamani kutembea kwa miguu mpaka Ikulu kwenda kumshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi alioufanya wa kuzuia visiondolewe.

Waliyasema hayo juzi wakati wa  mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mwanavala Kata ya Imalilo- Songwe kati ya wakulima na wafugaji wa wilaya hiyo.

Walisema kabla ya uamuzi wa rais walikuwa wanateseka kwa zidi ya miaka 12.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Nguvu Kazi Mwanavala ambao ni wakulima wa Mpunga, Juma Kanyamala, alisema kati ya vijiji na vitongoji 366 alivyovitaja rais na wao wameguswa kwa kiasi kikubwa.

Alisema asilimia kubwa ya wananchi wa Wilaya hiyo ajira yao ni kilimo na ufugaji na kudai kuwa endapo serikali ingeendelea na Tafsiri ya Tangazo lake namba 28 la mwaka 2008 (GN. 28) lililokuwa linafuta vijiji hivyo ajira zao zingekufa.

“Tuna furaha kubwa sana wakulima na wafugaji wa Mbarali na tungekuwa tunaweza tungeandamana kwa miguu mpaka ikulu tukamshukuru rais wetu, kwa sasa tunasubiri siku akifanya ziara Mbeya tutatembea mpaka eneo atakalokuwa anapokelewa,” alisema Kanyamala.

Alisema katika Skimu ya umwagiliaji ya Mnazi wakulima wanaolima wapo 460 lakini baadhi ya wasaidizi wa rais walikuwa wanasema wakulima hao hawazidi 50.

Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji wilaya ya Mbarali, Moses Fute, alisema kabla ya rais kutoa tamko la kutoondolewa kwa vijiji hivyo, wafugaji walikuwa wanaishi kama wakimbizi ndani ya ardhi yao.

Alisema kutokana na mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu, wananchi wa maeneo hayo walipoteza mali zao nyingi, wengine waliumia na wengine walipoteza maisha kwenye harakati za kugombea maeneo hayo.

Alisema wafugaji walikumbwa na changamoto za kufukuzwa katika maeneo hayo na kwamba awali walikubwa na operesheni iliyokuwa inajulikana kwa jina la ‘operesheni ondoa mifugo’ ambayo alidai ilisababisha mifugo yao kupotea.

 “Kuna wakati askari wa Tanapa walipiga risasi mifugo yetu ikafa lakini pia kuna wenzetu saba walipigwa risasi na watatu kati yao walifariki, sasa tumeshapata rais mkombozi ambaye ameona sisi tunastahili kuishi, nawaomba wenzangu tumshukuru kwa vitendo,” alisema Fute.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles