26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi Rombo waonywa kupuuza chanjo

Na Upendo Mosha, Rombo

MBUNGE wa Rombo, mkoani Kilimanjaro, Profesa Adolf Mkenda, amewaonya wananchi kuacha mara moja tabia ya kupuuza kuchoma chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 na badala yake kuiamini serikali na wataalam wa afya ili kupunguza kasi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Profesa Mkenda, aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mradi wa matundu 16 ya vyoo vya wanafunzi na waalimu katika shule ya msingi Mbomai Juu, Kijiji cha Mbomai, kata ya Tarakea Motamburu, wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Alisema wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakipuuza kuchoma chanja ya covid 19 licha ya wilaya hiyo kuathirika zaidi na vifo vingi vitokanavyo na ugonjwa huo na kwamba ni vema wakawaamini wataalamu wa afya na serikali na kuchanja na kupuuza upotoshaji.

“Covid ipo na imeua sana Rombo na sababu ni kutokana na wilaya hii kuwa na mwingiliano mkubwa wa watu, kila siku magari zaidi ya 10 yanaondoka kwenda mikoani, watu wetu pia ni wajasiriamali wanakuja na kutoka hivyo maambukizi hapa ni mengi mno, chanjo ni hiari ila naomba mchanje.

“Waaminini wataalamu wa afya na serikali maana mnapougua mnaenda hosptali na anayeamua dawa gani utumie ni Daktari sasa wataalamu hao hao ndo wanawaambia mchanje mnabisha,mkichanja wengi mtaokoa wengi, mimi nimechanja na familia yangu na viongozi wengi tu naomba mchanje,” alisema Profesa Mkenda.

Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Kilimo,.alisema ni vema wananchi hao wakapata chanjo hiyo jambo ambalo litasaidia kupunguza uwezeno mkubwa wa kuambukizwa na kuambukiza na kupunguza vifo na kwamba upotoshaji unaoendelea kwamba chanjo hiyo inamadhara hauna afya na ni wa kupuuza.

“Inasikitisha kuona idadi ya waliochanja Rombo ni ndogo Sana ndugu zangu mchanje,wazungu hawawezi kutuua ili waje kuchukua nini viamba? dawa nyingi zinatoka kwao pia chanjo za watoto wanatoa hadi bure, sisi tulichanja chanjo ya pepo punda leo mnaogopa chanjo ya covid 19, chanjeni hasa wale wenye umri wa miaka zaidi 50,”alisema

Mbali na hilo, Profesa Mkenda aliahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya paa na madarasa kwa awamu tofautitofauti Jambo litakalo wawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo,Kanal Hamisi Maigwa,alisema wananchi waliopata chanjo ni zaidi ya watu 2,000 na kwamba bado mwitikio ni mdogo na elimu zaidi inahitajika kuhamasisha wananchi kuona umuhimu wa kuchanja.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mkuu wa shule hiyo, Lucy Massawe, alisema jumla ya Sh mil 34.5 zikitumika kujenga vyoo hivyo vyenye matundu 16,fedha zilizotokana na michango ya wananchi,mfuko wa Jimbo na wafadhili mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles