Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Baadhi ya Wananchi waliosalia ndani ya mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro (NCAA) wamesema kuwa wanaishi katika maisha ya tabu yasiyokuwa na huduma za kijamii na kwamba wanatamani kuondoka.
Wakizungumza na waandishi wa habari Agosti 13, 2023 katika kata za Nainokanoka na Naiyobi, wameeleza kuwa wanataka kuondoka kwa hiari kuwafuata wenzao katika makazi mapya ya Msomera huku wakiiomba Serikali ya Rais Dk. Samia ifanye hivyo haraka kwa kuwa hawaoni sababu ya kuendelea kuishi katika maeneo hayo.
Sinyati Emmanuel na Marry Kesumo wamesema hawawezi kuishi mahali ambapo hakuna bara bara nzuri, maji,hospitali wala usafiri na kwamba hawana shughuli za maendeleo wanazozifanya kwa kuwa hawaruhusiwi hata kulima katika maeneo hayo.
Naye, Jennifer Yuda kutoka kijiji cha Kapenjiro kata ya Naiyobi ambaye yupo tayari kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, ameiomba Serikali iwapatie maeneo kutokana na idadi ya Wake waliopo katika Boma husika.
Mosses Lenara ameishukuru Serikali kwa upendeleo ilioutoa kwao kwa kuwajengea nyumba Msomera na kuwapatia maeneo ya kilimo na ufugaji.
Serikali ilitoa nafasi ya kuwahudumia kila kitu ikiwa ni pamoja na kuwajengea Nyumba, Shamba na maeneo ya malisho, kuwasafirisha wao, mifugo na mizigo yao wote waliokubali kuhamia Msomera mkoani Tanga kwa hiari ili kupisha eneo hilo ambalo ni makazi ya wanyamapori wanaoingizia nchi mapato kupitia watalii.