27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 12, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania, Malawi kushirikiana kuzalisha umeme Mto Songwe

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Tanzania na Malawi zimekubaliana kushirikiana katika uzalishaji umeme wa megawati 180 kwa kutumia maporomoko ya Mto Songwe.

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, akizungumza baada ya ujumbe wa Serikali ya Malawi kutembelea Kituo cha Kuchakata Gesi Asilia cha Kinyerezi 1. Watatu kushoto ni Waziri wa Nishati Malawi, Ibrahim Matola.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Agosti 11, 23 kufuatia maelekezo ya marais wa nchi hizo, Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Lazarus Chakwera walipokutana hivi karibuni.

Rais Samia alifanya ziara nchini Malawi Julai 5, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao walikubaliana kuendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali kudumisha uhusiano uliopo.

Wakizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo Dar es Salaam, Waziri wa Nishati, January Makamba na Waziri wa Nishati Malawi, Ibrahim Matola, wamesema yataleta manufaa kwa nchi zote mbili.

Waziri Makamba amesema makubaliano hayo pia yatahusisha ujenzi wa miundombinu ya umeme.

Amesema kutakuwa na kamati ya pamoja ya mawaziri na kamati ya wataalam ambapo kila upande utateua wataalam na vikao vitaanza rasmi Oktoba mwaka huu.

“Kutokana na maelekezo ya viongozi wetu Rais Samia Suluhu na Rais Chakwera walikubaliana tuongeze maeneo ya ushirikiano hasa eneo la nishati.

“Huu ni sehemu ya mradi wa kikanda wa kuwa na gridi moja katika kanda hii. Tunaamini miradi hii itanufaisha nchi zetu kwa sababu mahitaji ya umeme bado ni makubwa, ushirikiano huu utaimarisha uhusiano kati ya nchi zetu,” amesema Makamba.

Amesema pia upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga njia ya kusafirisha umeme itakayounganisha nchi hizo tayari umekamilika na sasa wanatafuta fedha uanze kutekelezwa.

Aidha amesema kamati ya wataalam itaamua eneo sahihi la mradi kutokana na taarifa za kiufundi zitakazopatikana.

Naye Waziri wa Nishati Malawi, Ibrahim Matola, amesema nchi nyingi Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki bado hazina nishati ya kutosha hivyo ni muhimu kuwe na miradi mingi zaidi katika sekta hiyo.

“Makubaliano haya ni mwanzo wa safari yetu ya kushirikiana katika nyanja nyingi. Rais Samia na Rais Chakwera walikubaliana kushirikiana pamoja kwa manufaa ya mataifa haya. Ni muhimu tuwe na miradi mingi zaidi katika sekta ya nishati,” amesema Matola.

Nchi hizo pia zimekubaliana kushirikiana katika eneo la gesi ambapo Tanzania inatarajia kuuza gesi Malawi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles