23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Dawasa mbioni kutekeleza myradi wa kuchakata maji taka Dar

Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetaja miradi ya kipaumbele kwa mwaka 2023-2024 katika Jiji la Dar es Salaam.

Miradi hiyo imetajwa leo Ijumaa Agosti 11,2023 na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, Kiula Kingu wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2023-2024.

Kaimu Mtendaji huyo amesema katika Wilaya ya Kinondoni na Ilala, miradi ya kuchakata majitaka itajengwa maeneo ya Mbezi Beach na Buguruni.

Amesema mradi wa Mbezi Beach unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya
Serikali na Benki ya Dunia ambapo jumla ya Sh bilioni 132.3 zitatumika kujenga
mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kuchakata lita milioni 16 kwa siku.

Aidha, mradi mwingine ni wa kujenga mfumo wa kukusanya majitaka na maeneo nufaika katika awamu hii ni Mbezi Beach, Kilongawima, baadhi ya maeneo ya Kawe na Salasala.

Amesema utekelezaji wa mradi umeanza na Wakandarasi wanaendelea na shughuli za maandalizi ya ujenzi.

Amesema DAWASA pia imekuja na ubunifu wa kujenga mifumo na mitambo midogo midogo ya kuchakata majitaka inayojengwa maeneo ya pembezoni ambapo zaidi ya lita 780,000 za majitaka zitakuwa zikichakatwa kwa siku.

“Miradi hii ambayo pia itajumuisha ujenzi wa vyoo vya umma 30, itasaidia kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hizi muhimu na hivyo kuboresha usafi wa mazingira,” amesema

Aidha, miradi hiyo itasaidia wananchi kupata huduma za usafi wa mazingira kwa gharama nafuu karibu na maeneo wanayoishi. Amesema wakandarasi wanaotekeleza miradi wanaendelea na ujenzi.

Amesema gharama za miradi hiyo ni Sh bilioni 25.7 na wanufaika wa miradi hii wanakadiriwa kufikia milioni 1.8.

Kaimu Mtendaji huyo amesema Dawasa imejipanga kuendelea kuboresha upatikanaji wa
huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati saba ikiwemo mradi wa
ujenzi wa bwawa la Kidunda na Mradi wa ujenzi wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji.

Vilevile, mradi wa maji Kwala, mradi wa maji Mji wa Pangani Kibaha, ujenzi wa mradi kutoka Kimbiji-Kigamboni hadi jirani na Chuo cha Uhasibu T.I.A.

Pia,ujenzi wa mradi wa maji Kusini
mwa Jiji la Dar es salaam na Mradi wa uchimbaji visima virefu tisa eneo la Kigamboni.

Amesema Miradi hiyo itakayotekelezwa kwa jumla ya Sh bilioni 425.9.

Amesema miradi hiyo inalenga katika, kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa na DAWASA, kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuimarisha mfumo wa usambazaji maji na kuimarisha huduma katika maeneo ambayo hayana mtandao hasa yale ya pembezoni.

“Utekelezaji wa Miradi ya Usafi wa Mazingira kuboresha afya na mazingira pamoja na kuwekeza nguvu katika utoaji wa huduma za majisafi,”amesema Kaimu Mtendaji huyo.

Amesema DAWASA imejipanga kikamilifu na kuchukua hatua za makusudi za kuboresha usafi wa mazingira kupitia miradi mikubwa na midogo.

“Hii ni kwasababu upatikanaji wa maji unapoongezeka unapaswa uambatane na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira,”amesema Mtendaji huyo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles