Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila, akiwa na familia yake akipiga kura ya kuchagua rais mpya wa nchi hiyo mjini Kinshasa jana.
KINSHASA,Congo DRC
MAMILIONI ya wananchi jana walijitokeza kupiga kura nchini hapa katika uchaguzi wa kihistoria, baada ya kucheleweshwa kwa miaka kadhaa.
Uchaguzi wa rais unatazamiwa kuleta mabadilishano ya kwanza ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1960.
Katika uchaguzi Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwa madarakani tangu kuuawa kwa baba yake mwaka 2001, ataachia ngazi katika hatua ya kihistoria kwa taifa ambalo limeshuhudia utawala wa kiimla, mapinduzi ya kijeshi na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu lilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji.
Kukubali kwake kuheshimu ukomo wa mihula kunawakilisha hatua mbele kwa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Kwa mujibu wa kituo cha runinga cha Aljazeera vituo vya kupigia kura vilifunguliwa tangu saa 12:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni.
Kituo hicho kilieleza kwamba kulikuwa na idadi ndogo ya wapiga kura, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mapema jana kabla ya kazi hiyo ya upigaji kura kuanza.
Wakati hayo yakijiri Emmanuel Ramazani Shadary ambaye amesimamishwa na Rais Kabila kuwa mrithi wake kupitia Chama Cha FCC na Martin Fayulu wa Chama Kikuu Cha Upinzani cha UDPS, walipiga kura katika kituo kimoja mjini hapa.
Kiongozi upinzani atamba kushinda
Mara baada ya kupiga kura kiongozi huyo mkuu wa upinzani aliliambia Shirika la Habari la Ungereza Reuters kwamba ana uhakika wa kupata ushindi katika uchaguzi huo.
“Tangu usiku wa leo nina imani nitakuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,”kiongozi huyo aliwaambia waandishi wa habari.
Katika hotuba hiyo, Fayulu alisema uchaguzi huo umeonesha kumalizika kwa utawala wa Kabila.
“Kwa kura hii, sio kwamba tumemaliza tu shida za watu wa Congo bali pia itarejesha amani kwa watu wake na kuleta mageuzi kupitia uchaguzi huu,”aliongeza kiongozi huyo.
Hata hivyo wakati viongozi hao wakipiga kura mjini hapa ambako ni makazi ya wapiga kura zaidi ya milioni nne kuna taarifa zinazoeleza kuwa asilimia 20 ya vituo vya kupigia kura havikufunguliwa kutokana na uhaba wa vifaa vya kielektroniki.
Wapiga kura wanena
Taarifa ya kituo hicho ilieleza pia kuwa tofauti na ilivyokuwa ikidhaniwa na wengi kuwa mfumo wa upigaji kwa njia ya kielektroniki itawasumbua wengi.
Lakini hali hiyo imeonekana kuwa tofauti kwani baadhi waliongea na Aljazeera walieleza kuwa ilikuwa ni kazi rahisi.
“Ni kazi rahisi. Mwanzo nilidhani kitakuwa kitu kigumu, lakini kumbe sio. Ilinichukua chini ya dakika moja.Uchaguzi kwa njia hii ni wa haraka na rahisi kiasi cha kwamba sijawahi kuona,” Peter Ekoto alikiambia kituo hicho mara baada ya kupiga kura katika Manispaa ya Bumbu iliyopo mjini hapa.
Mpiga kura mwingine aliyongea na Aljazeera ni Micheline Kabund ambaye ni mwalimu alisema kuwa naye alikuta upigaji kura kwa mfumo huo ni kazi rahisi ingawa alitia shaka kutofahamu kilichopo ndani ya chumba.
Hata hivyo maoni ya wapiga kura hayo yalienda tofauti na mpiga kura mwingine, Blandine Kiemba ambaye alisema kwamba teknolojia hiyo inaweza kuwa mtihani mkubwa kwa wasiojua kusoma ama kutumia kompyuta.
*Wengine wakosa majina yao vituoni
Katika Manispaa ya Bumbu, vituo 10 kati ya 12 vilifunguliwa mapema, lakini baaadhi ya wapiga kura walishindwa kufanya hivyo baada ya kukosekana majina yao.
Mmoja wa wapiga kura hao, Aristote Zenga ambaye kazi yake ni dereva alisema kuwa alishindwa kutumia haki yake baada ya kukuta jina lake halimo kwenye orodha ya wapiga kura licha ya kuwa alijiandikisha.
Uchaguzi huo pia hakufanyika katika miji mitatu kama ilivyotangazwa na Tume ya Uchuguzi, (CENI) ambapo katika miji ya Beni na Betumbo iliyopo Kaskazini Magharibi mwa Jimbo la Kivu umesogezwa mbele hadi Machi mwakani kufuatia kuwapo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao umeshaua watu zaidi ya 330 huku katika mji wa Yumbi uliopo Jimbo la Bandundu ukisogezwa hadi mwezi huo kufuatia kuendelea kuwapo kwa mapigano ya kikabila ambayo yameshagharimu maisha zaidi ya watu 100.
DRC ina zaidi ya watu milioni 80 ambao hawajawahi kuona kubadilishana madaraka kwa amani tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1960 . Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa Januari 15, 2019.