Safina Sarwatt, Moshi
ZAIDI ya wananchi 700 na taasisi za elimu, afya katika vijiji vya Koresa na Uchira wilayani Moshi, wamekosa huduma ya maji kwa zaidi ya wiki moja kutokana na kuibuka kwa mzozo kuhusu uhalali wa bodi mbili za maji.
Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo jana, walisema kwa zaidi ya wiki moja sasa hakuna huduma za maji hali inayochangia wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Koresa, Anna Matoi, alisema wanateseka kutokana na kukosa huduma ya maji wakati wao ndiyo waliotoa nguvu zao kwa kuchimba mitaro kutoka misituni hadi kwenye matanki.
“Bodi ya maji ya Kirua Kahe haitupi maji inavyostahili na wangekuwa watupa tusingehangaika kama hivi kutafuta maji na huenda hata yanayofanyika hapa kuna hujuma ndani yake.
“Kwa hali hii tunaziomba mamlaka za serikali akiwamo mkuu wa wilaya kuingilia kati suala hili,” alisema Matoi .
Naye mkazi wa Kijiji Cha Uchira, Hamisi Mvungi, alisema kinachondelea ndani ya bodi za maji za Kirua Kahe Mtiririko ni kuihujumu Bodi ya Watumia maji Uchira ili kuiua.
Alisema wananchi ndiyo waliounda jumuiya yao kwa lengo la kurahisha upatikanaji wa huduma ya maji hivyo aliiomba serikali kuingilia kati suala hilo.
“Wananchi walitoa maeneo yao kwa ajili ya mradi huu wa maji na mkataba unasema wananchi tutapewa maji kwa blaki mita yaani kwa usomaji wa mita za maji yanayopita kwenye matanki kwa mwezi.
“Lakini tunashangazwa na sintofahamu inayoendelea ndani ya hizi jumuiya mbili zinazohudumia wananchi,” alisema Mvungi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Watumia Maji Uchira, Lazaro Mfinanga, alikiri kuwapo tatizo hilo.
Alidai linasababishwa na Bodi ya Maji Kirua Kahe Mtiririko kuhujumu Jumuiya ya Watumia Maji Uchira hali ambayo inasababisha adha kubwa kwa wananchi.
“Kuna hujuma inaendelea ndani ya bodi ya maji ya Kirua Kahe Mtirirko wamekuwa wakifunga maji ili maji yasiingie kwenye matanki.
“Lengo lao ni kuhakikisha wanaiua Jumuiya ya Watumia Maji ya Uchira,” alisema Mfinanga.
Meneja wa Bodi ya Maji ya Kirua Kahe Mtiririko, Mambeya Mshana, alikiri kuwapo tatizo la ukosefu wa maji katika vijiji hivyo.
Alisema linasabaishwa na uharibifu wa miundombinu kwenye matanki yanayosambaza maji kwenye vijiji hivyo.