23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WANAJESHI 14 JWTZ WAUWAWA DRC

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WANAJESHI 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  waliokuwa kwenye  kikosi cha kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameuawawa  na wengine wawili hawajulikani walipo .

Taarifa zilizoripotiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana zilieleza kuwa, wanajeshi hao waliuwawa baada ya kambi yao ya Semuliki iliyopo eneo la Beni katika Mkoa wa Kivu Kaskazini kuvamiwa na waasi  mashariki mwa nchi hiyo juzi jioni.

Kumekuwa na taarifa za kukanganya kuhusu idadi ya wanajeshi wa JWTZ waliouwawa katika tukio hilo, wakati taarifa ya awali  iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN) ikisema kuwa ni 12, ile iliyotolewa na Ikulu ya Rais Dk. John Magufuli ilisema 14.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya UN, wanajeshi wengine 53 wamejeruhiwa baadhi yao hali zao zikitajwa kuwa ni mbaya.

Tukio hilo limeelezwa kuwa ni baya zaidi kuwahi kutekelezwa na waasi  dhidi ya walinda amani wa UN katika historia yake miaka ya karibuni.

Katika kipindi cha miezi sita tukio hili ni pili kutokea baada ya Oktoba mwaka huu wanajeshi wawili wa JWTZ  waliokuwa katika kundi la walinda amani  kuripotiwa  kuuawa na wengine 18 kujeruhiwa.

Mbali na hao,  askari wengine wawili pia waliripotiwa kuuawa  mwezi Mei, 2015 katika eneo la Kivu Mashariki mwa Kongo  na wengine wawili hawakujulikana walipo  baada ya kuvamiwa na waasi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alithibitisha kutokea kwa tukio hili la sasa kupitia  taarifa ambayo ilinukuliwa na BBC.

Guterres alishutumu vikali shambulio hilo na kulifafanisha na uhalifu wa kivita  na kuitaka  Kongo kufanya uchunguzi haraka na kisha  kuwawajibisha waliohusika.

Akielezea shambulio hilo, Guterres alisema ni baya zaidi kuwahi kutekelezwa dhidi ya walinda amani wa UN katika historia yake miaka ya karibuni.

“Ningependa kueleza kusikitishwa kwangu na shambulio hilo lililotekelezwa usiku wa jana (juzi) dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo,”.

“Taarifa za mwanzo mwanzo eneo la shambulio huko Kivu Kaskazini zinaonesha takribani walinda amani 12 kutoka Tanzania waliuwawa na wengine 40 kujeruhiwa, wanne vibaya,na tunafahamu pia kwamba wanajeshi watano wa Jeshi la Kongo waliuawa ,”alisema Guterres.

Umoja wa Mataifa umewatuhumu waasi wa Allied Democratic Forces  (ADF) kwa kutekeleza shambulio hilo.

“Natuma salamu zangu za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa wanajeshi wa kulinda Amani na wanajeshi wa FARDC waliouawa au kujeruhiwa,” alisema mwakilishi mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo ambaye ndiye pia mkuu wa kikosi cha walinda amani ambacho hufahamika sana kama Monusco.

Baada ya kutokea shambulio hilo, Umoja wa mataifa ulituma wanajeshi zaidi eneo hilo huku kamanda wa kikosi cha kulinda amani akitekeleza shughuli ya kuwaondoa majeruhi.

Awali, Katibu Mkuu Msaidizi wa UN, Jean-Pierre Lacroix anayeshughulikia masuala ya kulinda amani alikuwa ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba “idadi kubwa ya wanajeshi walikuwa wameuawa,”.

Pierre alisema wanajeshi zaidi walikuwa wametumwa kwenda eneo hilo na majeruhi walikuwa wanasafirishwa.

Kutokana na taarifa hizo, Rais  Dk. John  Magufuli  katika taarifa yake kwenye vyombo vya habari alisema amepokea kwa mshtuko na masikitiko  makubwa  taarifa  za  kuuawa kwa askari hao waliopo katika operesheni ya ulinzi wa amani katika nchini  humo.

Taarifa iliyotolewa jana  na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson  Msigwa ilieleza kuwa,  wanajeshi wa Tanzania waliojeruhiwa katika tukio hilo walikuwa ni 44.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la KujengaTaifa Dk. Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,  Jenerali  Venance Mabeyo, maafisa na maaskari wote wa JWTZ  pamoja na  familia za marehemu na watanzania wote kwa kuwapoteza mashujaa waliokuwa wakitekeleza wajibu wao.

Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya vijana wetu, askari shupavu na mashujaa waliopoteza maisha wakiwa katika majukumu ya kulinda amani kwa majirani zetu DRC, alisema Dk.Magufuli.

Rais Magufuli pia amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kawaida.

Zaidi amewataka Watanzania wote kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua zinazostahili baada ya kutokea tukio hilo.

Tukio hili limetokea wakati taarifa za UN zinaonyesha  kuwa, kikosi hicho kinacholinda amani nchini Kongo ndicho kikubwa zaidi duniani kote.

Kwa mujibu wa taarifa hizo za UN, hadi sasa askari wa waliouwawa tangu  mwaka 1999 wanakadiriwa kufikia 300.

Tangu wakati huo kiasi cha dola za Marekani bil 8.74 zimetumika kugharamia shughuli za kusaka amani katika eneo hilo la Mashariki ya Kongo na inakadiriwa askari 95,000 wamekuwa wakifanya kazi hiyo chini ya mwamvuli wa UN  wakitoka katika mataifa 30 duniani ikiwamo Tanzania.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles