25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wanahabari watakiwa ‘kujinoa’

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wadau wa Tasnia ya Habari nchini wamewataka Waandishi wa habari kusoma sheria zinazohusu masuala ya habari na nyingine ili wanapotaka zirekebishwe wawe na ushawishi mkubwa kwa watunga sheria na jamii.

Wito huo umetolewa Oktoba 21, 2022 na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wahariri juu ya mipango ya uchechemuzi wa mabadiliko ya sheria za habari.

Salim amesema kuwa mwandishi wa habari akijua haki zake, sheria zinazoongoza tasnia ya habari ataweza kukutana na makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wabunge na kuwashawishi juu ya sheria zinaminya uhuru wa habari na haki za binadamu.

“Bado waandishi hatujawa na uelewa mpana wa sheria zinazotuhusu, tufanye jitihada kuzijua. Tuwashawishi wenzetu juu ya sheria zinazokwaza ukuaji wa tasnia ya habari na maendeleo ya Taifa,” amesema.

Naye Mwezeshaji Tumaini Mbibo, amesema ni muhimu kwa waandishi wa habari kujua kiini cha matatizo yanayolikabili Taifa na njia za kutumia ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo husika.

Amesema haki za binadamu zinakwenda sambamba na demokrasia hivyo uwepo wa sheria zinazominya tasnia ya habari zinakwamisha maendeleo hivyo vema ikafanyika mipango ya kufanya ushawishi wa mabadiliko.

Naye, Sylvester Hanga amesema waandishi wa habari wanataka sheria za masuala ya habari ziwe rafiki ili zichochee demokrasia, haki za binadamu na maendeleo kwa Taifa.

Naye Joyce Shebe amesema anaamini wahariri wakijua namna ya kushawishi watunga sheria, sera na mipango ya Taifa watakuwa kwenye nafasi njema ya kuchochea maendeleo ya mtu mmoja na Taifa.

Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema wataendelea kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya sheria zinazogusa tasnia ya habari kwa kushirikiana na wadau wengine.

“Tunajipanga kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutatua matatizo yetu na yanayotukabili jamii, hatuwezi kutaka marekebisho ya sheria pasi na kushirikiana na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles