NAIROBI, KENYA
WANAFUNZI wenye hasira wameteketeza kwa moto shule 70 za sekondari katika mfululizo wa uharibifu wa mali za umma unaoendelea hapa tangu mwaka 2007.
Waziri wa Elimu, Fred Matiangi ameiambia Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza wimbi hilo kuwa hakuna hata wanafunzi 20 waliohukumiwa kwa kuteketeza mali ya umma, kwa sababu moja au nyingine kati ya visa 317 vilivyoripotiwa kati ya mwaka 2007 na 2016.
“Endapo Serikali itachukua hatua dhidi ya wale watakaoteketeza mabweni au hata madarasa yao, bila shaka waigaji wa vitendo hivyo wataogopa.
“Mara nyingi tumegundua zile shule ambazo zinachunguzwa kwa sababu ya wizi wa fedha za kufadhili masomo ya bure na fedha za kununulia vitabu vya wanafunzi, zinateketezwa kwa sababu zisizo na msingi,” alisema Matiangi.
Kwa mujibu wa taasisi inayosimamia walimu nchini Kenya (TSC), walimu 15 wakuu wanachunguzwa kwa matukio hayo.
Wadau wa masuala ya elimu nchini Kenya akiwamo Katibu Mkuu wa Muungano wa Walimu (KNUT), Wilson Sosion, wamelaumu mabadiliko ya sera yaliyotolewa na wizara ya elimu kuwa sababu ya machafuko hayo.
Sosion alidai kuwa miongoni mwa mabadiliko hayo, ni kuongeza muda wa muhula wa pili, na kupiga marufuku likizo ya kati ya muhula ujao na kupiga marufuku wazazi kuwatembelea wanafunzi shuleni kama sababu zinazochochea wimbi hili la moto shuleni.
Hata hivyo, Waziri Matiangi akijitetea aliiambia kamati hiyo ya Bunge kuwa kabla ya mabadiliko hayo kutangazwa, shule 90 zilikuwa tayari zimeteketezwa kwa moto.