Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wanafunzi watano wenye ulemavu wa viungo na akili wanaosoma katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Chang’ombe – Dar es Salaam wanaandaliwa kuwa walimu wa ufundi baada ya kufanya vizuri katika masomo yao.
Wanafunzi hao Sadick Olomi, Mohamed Seleman, Paulo Ngunyari, Mohamed Mussa na Paulo Mweta walijiunga na Veta kwa masomo ya ufundi wa kuunganisha vyuma na wameonyesha uwezo mkubwa.
Akizungumza na Mtanzania Digital mmoja wa walimu katika kitengo cha kufundisha watu wenye ulemavu, Kintu Kilanga, amesema katika darasa la wanafunzi 24 wa ufundi vyuma watano ndiyo wameonyesha uwezo mkubwa.
“Tuko wachache na kama mimi nimebakiza miaka michache kustaafu sasa nikitegema walimu wa kwenda kutafuta tunaweza kupata taabu kidogo, hapo unavyowaona (yaani wanafunzi hao) wengine wana miaka minne hapa na wengine wana miaka sita na naendelea kuwapika,” amesema Mwalimu Kilanga ambaye amefundisha wanafunzi wenye ulemavu kwa miaka 12 sasa.
Mwalimu mwingine katika kitengo cha kufundisha watu wenye ulemavu Emmanuel Bukuku, amesema wanafunzi hao wameshiriki katika kutengeneza vitu mbalimbali ikiwemo maabara inayotembea ya Fizikia ambayo kwenye mashindano ya Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika jijini Dodoma ilishika nafasi ya kwanza.
“Tumeshirikiana nao kwenye kazi nyingi sana na ukimuelekeza anafanya vizuri, mfano kazi unazoona hapa (anamuonyesha mwandishi) nyingi tumeshirikiana nao. Maabara ya Fizikia inayotembea wameshiriki kwa asilimia kubwa, wazazi wasiwadharau wanaweza.
“Kama kwenye jamii kuna watoto kama hawa wawalete VETA, wanapokuwa majumbani wanatengwa, wanabaguliwa kwahiyo hata kisaikolojia wanaathirika. Wanapokuwa wengi pamoja na wale wengine huwa wana – ‘change’ yaani anakuwa tofauti na alivyokuja nimeona hicho kitu. Kwa hiyo ni tiba mojawapo kwenye upande wa ufahamu na akili,” amesema Mwalimu Bukuku.
Mmoja wa wanafunzi hao Paulo Ngunyari, ambaye ana ulemavu wa viungo amesema ana miaka minne katika chuo hicho ambapo alijiunga baada ya kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Pugu na kwamba malengo yake ni kuwa mwalimu ili awasaidie wengine.
“Ulemavu si laana, si ugonjwa na wala si bahati mbaya ni hali ambayo mtu yeyote anaweza akapata hivyo wajikubali waamue kufanya vitu inawezekana,” amesema Ngunyari.
Kwa upande wake Witness John ambaye ni mzazi wa Paulo Mweta, amesema baada ya kumpeleka mwanawe katika chuo hicho amebadilika na kuchangamka tofauti na alivyokuwa awali.
“Kwa kweli namshukuru Mungu na hasa hasa walimu, Paulo amebadilika sana anatengeneza majalo, mabanio na vitu vingine vingi tu anauza,” amesema Witness.
Katika karakana ya ufundi wa kuunganisha vyuma mwandishi wa habari hizi alipofika alipokelewa na Paulo na kuanza kumuonyesha vitu alivyotengeneza pamoja na maabara inayotembea ya Fizikia ambayo yeye na wenzake wameshiriki kuitengeneza.
“Karibu sana mimi naitwa Paulo John Mweta hapa tunatengeneza vitu vingi kama hili kopo la kuogea (anamuonyesha mwandishi huku akiwa ameliweka kichwani kwake kama vile anajimwagia maji), hizi unazijua (yaani chuma za kuchomea nyama) nimetengeneza mimi, na ile maabara wote hapa unaotuona tumetengeneza,” amesema Mweta.