WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Kafisha wilayani Tanganyika, Mkoa wa Katavi, wanalazimika kusomea masomo yao chini ya miti ya miembe kutokana na shule hiyo yenye mikondo saba kuwa na madarasa mawili ya kusomea .
Hayo yalisemwa juzi na Diwani wa Kata ya Ikola, Philimoni Moro (CCM), alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazoikabili kata hiyo iliyoko mwambao mwa Ziwa Tanganyika.
Alisema shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 600 na ina vyumba viwili vya madarasa, huku ikiwa na mikondo ya kuanzia darasa la kwanza hadi la saba pamoja na walimu saba.
Diwani Moro alisema kipindi cha mvua za masika kimekaribia kuanza, hivyo hajui wanafunzi wa shule hiyo watakuwa wanasomea wapi kwa kipindi hicho.
“Pamoja na jitihada zilizofanywa na wananchi za kuchangia madawati katika shule hiyo, lakini wanavunjika moyo baada ya kuona madawati waliyochangia yakiwa yako nje yanapigwa na jua,” alisema.
Naye Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso (CCM), alikiri kuwepo kwa tatizo la upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa
Alisema tatizo hilo ni la muda mrefu ndiyo maana miaka mine iliyopita yeye kama mbunge aliweza kutoa msaada wa madawati kwenye baadhi ya shule ambazo wanafunzi walikuwa wakisomea chini na pia alichangia vifaa vya ujenzi wa majengo ya madarasa .