27.9 C
Dar es Salaam
Monday, February 26, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI WAPIGWA MABOMU

Na DERICK MILTON-BARIADI


JESHI la Polisi katika Wilaya ya Bariadi mkoani  Simiyu, jana liliwapiga mabomu ya machozi wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi waliokuwa wakiandamana kupinga Mkuu wa Shule yao, Deus Toga, kuhamishwa.

Wakati wa maandamano hayo yaliyofanyika saa 6.00 mchana wanafunzi hao wapatao 600, walifunga barabara kuu ya Bariadi – Lamadi.

Pia, shughuli mbalimbali za  jamii mjini Bariadi zilisimama kwa zaidi ya saa mbili kwa kuwa hakukuwa na utulivu.

Taarifa zilizopatikana zinasema   wanafunzi hao waliandamana wakipinga Mwalimu Toga kuhamishiwa katika Shule ya Sekondari Giriku.

Kabla ya wanafunzi hao hawajapigwa mabomu hayo, walianza kuandamana kuelekea ofisi ya Mkuregenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Merkzedek Humbe, ambaye ndiye aliyemhamisha Mwalimu Toga.

Wakati wakielekea ofisini kwa mkurugenzi huyo, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliwadhibiti kabla hawajafika walikokuwa wakielekea.

Taarifa zinasema   walipozuiwa kuelekea ofisini kwa mkurugenzi, walibadili mwelekeo na kuelekea ofisini kwa mkuu wa Mkoa wa Simiyu ili wakapeleke malalamiko yao.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wanafunzi hao walisambaratishwa na askari hao baada ya kufika jirani na Hospitali Teule ya Mkoa wa Simiyu iliyoko Somanda.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao wa kidato cha kwanza hadi cha sita, walilazimika kutanda katikati ya barabara ya Bariadi – Lamadi.

Wakiwa barabarani hapo, walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kutomtaka Mkuu mpya wa Shule yao, Paul Lutema, aliyepelekwa  kushika nafasi ya Mwalimu Toga.

Pamoja na nyimbo hizo, walikuwa pia wamebeba mabango mbalimbali yenye ujumbe tofauti yakiwamo yaliyosema ‘mlimleta kuinua elimu shuleni kwetu mnamuondoa’, ‘D.E. O’ ni jipu na mengine yalisomeka ‘tunamtaka mkuu wetu Toga’.

Baada ya kukaa kwa muda barabarani hapo, walianza kuwarushia mawe polisi waliokuwa wamewazunguka wasielekee ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Simiyu.

Polisi hao walipozidi kupigwa mawe, walilazimika kujibu mapigo kwa kuwarushia mabomu ya machozi   kuwatawanya wanafunzi hao.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema walifikia uamuzi huo baada ya kutangaziwa na mwalimu wao wa zamu kwamba Mwalimu Toga, alikuwa amehamishwa.

“Baada ya kutangaziwa hivyo, tuligoma kuingia madarasani na kuamua kuandamana kwenda ofisini kwa mkurugenzi na ofisi ya mkuu wa mkoa kutaka mwalimu wetu arudishwe kwa sababu ni mchapa kazi.

“Wanafunzi wanamtaka Mwalimu Toga kwa sababu tangu afike shuleni kwetu, ufaulu umeongezeka na migogoro ya shule iliyokuwapo imekwisha.

“Hata duka la shule lililokuwa limefungwa kutokana na migogoro ya walimu, limefunguliwa, ndiyo maana wanafunzi wanamtaka mwalimu huyo,” alisema mwanafunzi huyo.

Kutokana na hali ilivyokuwa, Kaimu Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga na Ofisa Elimu wa Mkoa, Julius Nestory, walifika  shuleni hapo kuwatuliza wanafunzi kwa kuzungumza nao.

“Kaimu mkuu wa mkoa aliwasihi wanafunzi warejee madarasani kuendelea na masomo kwa kuwa madai yao ya kumtaka Mwalimu Toga yalikuwa yamekubaliwa.

“Lakini ofisa elimu alisema ofisi ya mkurugenzi ilimhamisha Mwalimu Toga kwa makosa kwa sababu haikuzingatia sheria na taratibu za uhamisho kwa sababu mwenye mamlaka wa kuwahamisha wakuu wa shule ni Katibu Tawala wa Mkoa.

“Ofisi ya katibu tawala wa mkoa na ofisi yangu ya elimu, hatukuwa na taarifa za uhamisho huu. Kwa hiyo, tumeamua kuutengua na tunawataka viongozi wenzangu wasifanye uamuzi bila kufuata utaratibu na sheria,”alisema ofisa elimu huyo.

Mwalimu Toga alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo  alikataa kusema chochote ingawa alionyesha kushangazwa na uamuzi huo wa wanafunzi.

“Naomba nisizungumze lolote kwa sababu hata mimi nashangaa kusikia haya. Yaani sielewi ni nini kimesababisha yote haya mpaka wanafunzi kufikia uamuzi huu, niacheni,” alisema Mwalimu Toga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles