WANAFUNZI wa vyuo vikuu mbalimbali wameendeleza vilio kwa kukosa mikopo licha ya kuwa na vigezo vya kupewa mikopo huku wakiitaka serikali kuacha siasa katika suala la elimu.
Jana wanafunzi zaidi ya 100 wenye sifa za kupewa mkopo walikusanyika nje ya ofisi za Bodi kutaka kuonana na Mkurugenzi, Abdul- Razaq Badru ili awape sababu ya kuwabagua bila kuangalia uhitaji wao.
Vilio hivyo vimekuja ikiwa ni siku moja baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutoa ufafanuzi wa sifa za kupata mkopo ambazo zinawatenga wanafunzi waliosoma shule binafsi, diploma na waliochelewa kujiunga na vyuo vikuu kwa zaidi ya miaka mitatu baada ya kumaliza kidato cha sita.
“Tunaiomba serikali waache siasa katika suala la elimu,” alisema mmoja wa wanafunzi hao ambaye alijitambulisha kwa jina la Vaison Franco mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Rais kwa kinywa chake wakati wa kampeni alisema hakuna mtoto wa maskini atakayekosa mkopo, lakini leo hii tunawekewa vigezo vingine kutubagua sisi ambao tulisoma kwa tabu kwa kurudia mitihani, wengine QT (mtihani wa maarifa) na leo tumefika hapa unatuambia hautupi mkopo kwa sababu tumesoma shule binafsi,” alisema mwingine.
Mwanafunzi mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini wa Chuo cha Tumaini Dar es Salaam, alisema amefika kuiuliza Tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) kwa nini haikuweka vigezo vya wanaotakiwa kuomba mkopo wakati wanatuma maombi.
“Wakati tunaomba mikopo hawakutuambia kuhusu sifa hizi za kupata mkopo iweje leo ndio waje kutuambia kuwa hatupewi mkopo kwa sababu tumesoma diploma au shule binafsi.
“Ukiangalia wengi hapa tumesoma QT tena ndio tulipaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wengine wamesoma shule binafsi za hadi laki nne ambayo unatoa kwa awamu, iweje leo umweke kwenye kundi la matajiri bila kuangalia uwezo wa wazazi wake kiuchumi?” alihoji.
Naye Geofrey Wambura kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliitaka Serikali kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji na si kuangalia mtu alisoma wapi kwani wapo waliosoma shule binafsi kwa kusaidiwa na wahisani.
“Tunaomba Bodi ya Mikopo na serikali isikie kilio chetu sisi wanafunzi tuliosoma kwa kuunga unga ada, leo hii tunabaguliwa wakati Rais mwenyewe alisema mikopo ni kwa wote wanye uhitaji,” alisema Wambura.
Kwa nyakati tofauti MTANZANIA ilifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Bodi, Badru ambapo alieleza kuwa serikali kwa mwaka huu ina uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 25,717 tu kulingana na bajeti iliyopangwa.
Wakati mwaka huu serikali ikitoa mikopo kwa wanafunzi 25,717 wa mwaka wa kwanza, mwaka jana ilitoa mikopo kwa wanafunzi 54,072 wa mwaka wa kwanza ikiwa ni mara mbili zaidi ya sasa.
Hata hivyo duru za siasa zinaeleza kuwa kutolewa kwa mikopo kwa wanafunzi wengi mwaka jana kulifanyika kisiasa kutokana na kwamba ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi.