Na Mwandishi Wetu, Lindi
Taasisi ya Lorna Dadi kupitia Mradi wake wa Nisitiri (Dhamini Hedhi) imekabidhi taulo za kike zinazofuliwa kwa wanafunzi 200 wa shule za Sekondari za Milola na Kitomanga zilizopo Jimbo la Mchinga mkoani Lindi ili ziwasaidie kuhudhuria vipindi vya masomo pindi wanapokuwa katika hedhi.
Akipokea taulo hizo mjini hapa jana kwa niaba ya Mbunge wa Mchinga (CCM), Mama Salma Kikwete, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, amesema wanatambua juhudi za kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wa kike na maendeleo mbalimbali ya Mkoa wa Lindi zinazofanywa na mbunge huyo.
Juhudi zake tunaziona na tunatambua mchango wake katika kuleta maendeleo ya halmashauri yetu, tunaahidi kushirikiana naye kwa kila jambo, amesema Ndemanga.
Pia amesema ugawaji wa taulo hizo umekuja wakati mwafaka kwa kuwa Halmashauri ya Lindi iko katika mkakati maalumu wa kuzidisha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wote.
Taulo hizi zitawafanya wanafunzi wa kike wahudhurie masomo yao siku zote na kuwasaidia wafaulu vizuri katika masomo yao, amesema Ndemanga.
Katika hatua nyingine, amesema halmashauri hiyo iko katika majadiliano ya kina kuhakikisha shule mpya ya sekondari ya kidato cha tano na sita inajengwa katika Jimbo la Mchinga au zilizopo zinaboreshwa.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Lorna Dadi, Lorna Dadi, amempongeza Mama Salma kwa juhudi zake za kuwasaidia wananchi wa Mchinga na Lindi kwa ujumla na ameahidi kushirikiana naye bega kwa bega kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanafunzi hasa wa kike zinatatuliwa.