Na ANNAÂ RUHASHA,
WANAFUNZI wa Chuo cha Uuguzi wilayani Sengerema wameendelea na mgomo wa kuingia madarasani na wodini, imefahamika.
Hiyo ni baada ya wanafunzi wenzao 17 kufukuzwa chuoni hapo walipomweleza mkuu wa wilaya hiyo changamoto wanazokabiliana nazo,  wiki iliyopita.
Hayo yamebainika jana wakati waandishi wa habari walipotembelea chuoni hapo kutaka kupata ufafanuzi wa mgomo wa wanafunzi  tangu Novemba 29 mwaka huu.
Mkuu wa Chuo hicho, Samweli Mathew alisema  wanafunzi 17 wamefukuzwa katika chuo hicho akidai ndiyo vinara wa   mgomo ambao waliwalazimisha  wenzao zaidi 100 kushiriki.
Aliwataja waliofukuzwa chuoni hapo kuwa ni pamoja na Rais wa wanafunzi,  Godfrey Cosmas, Said Sabato, Deogratias Mjawa, Robinson Reuben, Elisha Tito, Chacha Werema, Martine Robert, Zephania Lazaro na Sophia Shija wote ni wanafunzi wa mwaka wa tatu.
Wanafunzi wa mwaka wa pili waliofukuzwa ni Toy Edward, Elizabeth Mashala, Rodrick Novati, Elasto Elias, Gelson Kakulu, Steven Siango na Crispini Kichaha.
Alisema uamuzi wa kuwafukuza wanafuzi hao ulifikiwa na bodi iliyokaa Desemba 8 mwaka huu.
Mathew alisema wanafunzi hao walifukuzwa wakidaiwa kukiuka maadili ya chuo.
‘’Baada ya kukaa bodi tuliona kwanza tuwaondoe hawa. Baada ya hapo nilizungumza na wanafunzi.
“Walionyesha kama wamenielewa lakini nashangaa mpaka sasa wameendelea kugoma,’’ alisema Mathew.
Hata hivyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Sengerema, Alani Mhina (DAS) alisema  wanafunzi waliofukuzwa siyo kwa sababu ya mgomo bali wamefuata ada.
Alisema endapo itabainika wamefukuzwa atautaka uongozi wa chuo kuwarudisha mara moja wanafunzi hao.
Wanafunzi waliobaki chuoni wameiomba serikali kukichunguza chuo hicho kwa tabia yake ya kuwaondoa wanafunzi wanaposema ukweli.